Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
4 September 2025, 5:14 pm

Chama cha Ushirika TUSHIKAMANE AMCOS kilichopo kata ya Mwaya, wilayani Ulanga mkoani Morogoro, kimewalipa wakulima 14 zaidi ya shilingi milioni 66 walizokuwa wanadai kwa msimu wa kilimo 2024, kwa kushirikiana na serikali ya wilaya kupitia Idara ya Kilimo.
Na: Isidory Mtunda
Chama cha Ushirika TUSHIKAMANE AMCOS kilichopo kata ya Mwaya, wilayani Ulanga mkoani Morogoro, kwa kushirikiana na serikali ya wilaya kupitia Idara ya Kilimo, kimefanikiwa kuwalipa wakulima 14 zaidi ya shilingi milioni 66 walizokuwa wanadai kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2024.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi malipo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Kaimu Katibu Tawala Hulka Rajabu, aliwataka wakulima kutokata tamaa, akisisitiza kuwa serikali ipo imara na inalinda haki za wananchi wake kupitia mifumo ya kisasa ya utunzaji kumbukumbu. Aliongeza kuwa, pamoja na kuchelewa kwa malipo, hakuna mkulima atakayepoteza haki yake.

Kwa upande wao, viongozi wa TUSHIKAMANE AMCOS, Katibu Yasini Ngwega na Mhasibu Ng’washi Nkwabi, waliishukuru serikali ya wilaya kupitia Idara ya Kilimo kwa kusaidia kufanikisha malipo hayo, na kuwapongeza wakulima kwa kuwa wavumilivu kipindi chote cha kusubiri malipo yao.
Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Morogoro, Bi. Sesilia Sostenesi, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga na Ofisi ya Mkurugenzi kwa usimamizi bora wa malipo hayo. Amesema kuwa mwaka huu wakulima wameuza kilo zaidi ya milioni tano za mazao mbalimbali, zenye thamani inayokadiriwa kuwa zaidi ya shilingi bilioni 11.
Wakulima Martina Marselino na Herege Pasanda Mwandu walipongeza juhudi za serikali baada ya kulipwa fedha zao, huku wakitoa rai ya kuboreshwa kwa mifumo ya malipo ili kuepusha ucheleweshaji kama uliotokea msimu uliopita.
Kupitia jitihada za serikali ya wilaya ya Ulanga na usimamizi wa idara ya kilimo, hatimaye wakulima hao wameweza kulipwa madai yao, hatua inayoashiria maboresho katika usimamizi wa vyama vya ushirika na uimarishaji wa mifumo ya malipo kwa wakulima vijijini.