Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
3 September 2025, 8:39 pm

Jeshi la Polisi licha ya kuwa na jukumu la kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia bado linahitaji usaidizi na ushirikiano wa jamii hasa kwenye uangalizi wa watoto
Na Katalina Liombechi
Katika kukabiliana na vitendo vya ukatili Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilombero kupitia Dawati la Jinsia na Watoto limezindua rasmi kampeni ya awamu ya pili ya Waambie Kabla Hawajaharibiwa, kampeni inayolenga kuwapa elimu ya kujilinda wanafunzi wanaotarajiwa kuhitimu elimu ya msingi mwaka huu.
Uzinduzi huo umefanyika leo mbele ya wanafunzi, walimu, na wazazi, ambapo maafisa wa Jeshi la Polisi wameeleza kwa kina madhara ya ukatili wa kijinsia, mimba za utotoni, ndoa za kulazimishwa, na matumizi ya dawa za kulevya vitendo vinavyotishia mustakabali wa watoto wengi hususan wa kike.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo akiwa katika Shule ya Msingi Mlabani Mkuu wa Polisi jamii Wilaya ya Kilombero Simpolianus Chacha amesema Kampeni hiyo inalenga shule zote za msingi katika Wilaya hiyo huku matarajio yao yakiwa ni kuona watoto wanakuwa wema,waadilifu na hawakumbani na madhila mbalimbali watakapokuwa majumbani.

Mwalimu Gaudence Mbanile kutoka shule ya Msingi Mlabani amesema elimu hiyo iliyotolewa na jeshi la polisi ni njia thabiti kwa watoto hao kujiandaa na maisha wakiwa nyumbani huku akitoa wito kwa wazazi kuwafuatilia kwa ukaribu ili wasiharibiwe kama ambavyo jeshi la polisi Kilombero limekusudia.
Baadhi ya Wanafunzi katika shule ya Msingi Mlabani wamelishukuru jeshi la polisi na kwamba elimu hiyo ni mfumo mzuri wa maisha kujiepusha na vitendo hatarishi huku wakiomba uendelevu wa elimu hiyo kwa watoto wengine.
Kampeni ya “waambie kabla hawajaharibiwa” awamu ya pili hii leo Septemba 3,2025 ikiwa ni siku ya uzinduzi wametoa elimu katika shule za Mtoni,Mlabani,Lipangalala na michenga,Na kesho Septemba 4 wataendelea katika shule zingine Tarafa ya Mang’ula lengo ni kuzifikia shule zote katika Wilaya ya Kilombero.