Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
28 August 2025, 11:44 am

Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Wakili Danstan Kyobya, ameagiza maafisa maendeleo ya jamii katika halmashauri zote kuhakikisha kila mmoja anakata vitambulisho 10 vya wajasiriamali ndani ya mwezi Septemba, ili kuhamasisha shughuli za ujasiriamali na kuwezesha wananchi kiuchumi.
Na; Isidory Mtunda
Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Wakili Danstan Kyobya, ameagiza wakurugenzi wa halmashauri zote kuhakikisha kuwa kufikia mwisho wa mwezi Septemba 2025, kila Afisa Maendeleo ya Jamii awe amekata vitambulisho 10 vya wajasiriamali.

Agizo hilo limetolewa katika Kongamano la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga, lililofanyika katika viwanja vya CCM Tangani, Halmashauri ya Mji wa Ifakara ambapo yeye alikuwa mgeni rasmi.
Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Kilombero wakili Dunstan Kyobya
Katika kongamano hilo, imebainika kuwa mwitikio wa uchukuaji wa mikopo ya asilimia 10 na kwa wafanyabiashara wadogo (WBN) bado ni mdogo ukilinganisha na kiasi cha fedha kilichoingizwa katika akaunti za halmashauri hizo, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi imeelezwa kuwa na mwitikio mdogo zaidi.

Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Morogoro, Saidi Mwakapugi, akitoa taarifa kwa mgeni rasmi, amesema Malinyi imetumia kiasi cha shilingi milioni saba tu kati ya shilingi milioni sabini zilizotengwa kwa mikopo hiyo.
sauti ya Said Mwakapugi, afisa maendeleo ya jamii mkoa wa Morogoro
Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Malinyi, Audifesto Liampawe, akizungumzia hali hiyo amesema changamoto kubwa ni uchache wa watumishi wa benki ya NMB katika wilaya hiyo, licha ya mzunguko mkubwa wa fedha mwaka huu ukilinganisha na miaka ya nyuma.
sauti ya afisa maendeleo halmashauri ya Malinyi, bwana Liampawe
Kwa upande wao, baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo kutoka halmashauri mbalimbali akiwemo Aidan Chungulu, Agnes Fyondi na Emanueli Selestin, wameishukuru serikali kwa mikopo hiyo wakisema imewasaidia kukuza mitaji yao, huku wakitoa wito wa kuongezewa kiwango cha mkopo.
sauti za wananchi walionufaika na mikopo
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkoa wa Morogoro, Mariana Emanuel Lutananurwa, amesema mkoa umejipanga kuboresha utekelezaji wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu vigezo na taratibu zinazopaswa kufuatwa kabla ya kuomba mikopo hiyo.

Ameeleza kuwa kati ya halmashauri zote za mkoa wa Morogoro, Halmashauri ya Mji wa Ifakara imeongoza kwa kutoa mikopo mingi zaidi kwa vikundi, ambapo jumla ya vikundi 35 vilinufaika kwa kiasi cha shilingi milioni 87 huku halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ikishika nafasi ya pili kwa kutoa mikopo kwa vikundi 28 yenye thamani ya shilingi milioni 68.
sauti ya Mariana Lutananulwa afisa maendeleo ofisi ya mkoa
Hadi kufikia Agosti 2025, hali ya utoaji wa mikopo katika baadhi ya halmashauri za mkoa ni kama ifuatavyo:
Halmashauri ya Mji wa Ifakara imeongoza kwa kutoa jumla ya shilingi milioni 87, ikiwafikia wafanyabiashara wadogo kupitia vikundi mbalimbali vilivyokidhi vigezo.
Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba (Mlimba DC) imetoa jumla ya shilingi milioni 61, ikishika nafasi ya pili kwa kiwango cha mikopo kilichotolewa.
Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 25.55, ikichochea juhudi za ujasiriamali vijijini.
Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi ndiyo imetoa kiasi kidogo zaidi cha mikopo, ambapo hadi sasa imetoa shilingi milioni 7.1 tu.
Tofauti hizi zimechangiwa na mambo mbalimbali, yakiwemo mwitikio wa wananchi, uelewa wa vigezo vya mikopo, changamoto za kiutendaji, na upatikanaji wa huduma za kifedha katika maeneo husika.
Kauli mbiu katika kongamano hilo; “UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI NI MSINGI WA MAENDELEO ENDELEVU”