Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
16 August 2025, 10:17 am

AWF wamekuwa wakitumia mbinu ya kushirikisha wadau wengine kuhifadhi Bonde la Kilombero wakiamini jitihada za pamoja ndizo zinaweza kusaidia kufikia malengo ya kurejesha mazingira ya asili katika eneo hilo muhimu
Na Katalina Liombechi
Mkoa wa Morogoro umeendelea kuonyesha dhamira na kuheshimu mchango wa wadau mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori Afrika (AWF), katika juhudi za serikali kuhifadhi mazingira na kuokoa Bonde la Kilombero – eneo muhimu kiikolojia linalotegemewa kwa uendelevu wa miradi mikubwa ya kimkakati kama bwawa la Mwalimu Nyerere.
Hayo yamebainishwa na Dkt. Rozaria Rwegasira,Katibu tawala Msaidizi Mkoa wa Morogoro wakati akikabidhi mfano wa hundi ya kiasi cha Shilingi Milioni 48, katika hafla maalum ambayo imefanyika Agosti 15, 2025, katika Ukumbi wa Edema Manispaa ya Morogoro,iliyoratibiwa na AWF.
Dkt. Rwegasira amesema kuwa Mkoa unajivunia kuwa na mshirika kama AWF, wenye dhamira ya dhati ya kushirikisha wadau mbalimbali kuhifadhi Bonde la Kilombero, eneo ambalo linathaminiwa sana kwa umuhimu wake wa ikolojia huku akiahidi kutoa ushirikiano wa karibu kutoka katika ofisi yake ili kuimarisha jitihada za kuhifadhi mazingira na kuendeleza miradi endelevu.

Hafla hiyo ilitanguliwa na semina kwa vinara wa uhifadhi wanaofanya kazi katika mandhari ya kilombero iliyoanza Agosti 14,2025 ambapo kwa mujibu wa Meneja wa Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori Afrika (AWF) amesema kuwezesha mafunzo hayo wameshirikiana na Chuo cha Kilimo SUA baada ya kuona mara zote wadau wanakuwa na mawazo mazuri lakini muda mwingine wanakwama kupata fedha kutokana na kushindwa kuandika maandiko ya miradi.
Katika hafla hiyo, AWF wamekabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 48 kwa taasisi za Mazingira alliance for community and Conservation (MACCO) ambayo imepata Tsh.Mil 23 na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa imepata Tsh.Mil 25 ikiwa ni taasisi zilizoshinda kati ya tisa zilizoshindania fedha hizo kuendeleza miradi bunifu ya uhifadhi.

Mratibu wa Taasisi ya Mazingira Alliance for Community and Conservation Felister Mwalongo amesema fedha hiyo wamekusudia kuendeleza miradi itakayokuza uchumi wa wakulima wa kokoa kwa kuwasaidia kupata elimu ya uchakataji na masoko lengo ni kuwafikia wakulima 200 katika vijiji vya Mngeta, Itongowa, Ikule, Kidete, Isago, na Mkangawalo.

Kwa upande wao Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa kupitia kwa Mhifadhi Mwandamizi Miraji Mramba amesema kuwa wanakwenda kutekeleza mradi wa kushirikisha jamii zinazopakana na hifadhi kwa kutoa elimu na mbadala wa kipato wananchi wanaolengwa ni kutoka vijiji vya Mwaya,Sanje na Mang’ula A ili kupunguza utegemezi wa rasilimali za hifadhi na kuondoa migongano kati ya jamii na wahifadhi.
Fedha hizo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Sustain-ECO, ambao AWF kwa kushirikiana na shirika la kimataifa linalojihusisha na uhifadhi wa Mazingira IUCN wanautekeleza kwa lengo la kurejesha mifumo ikolojia kwa kushirikisha wadau wengine wanaofanya shughuli za uhifadhi ikiwa ni mradi wa miaka mitatu unafadhiliwa na Serikali ya Sweden.