Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
11 August 2025, 7:27 pm

Serikali ya Tanzania imekuwa ikihamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kukabiliana na uharibifu wa mazingira na kuchochea uchumi kwa wananchi
Na Katalina Liombechi/Kuruthumu Mkata
Mradi wa teknolojia ya kutengeneza mkaa mbadala kwa kutumia mabaki ya kilimo cha mpunga wenye thamani ya Tsh. bilioni 2.5 kutekelezwa katika eneo la Ifakara unatarajiwa kuleta mageuzi ya kiuchumi ikiwa ni njia ya kuongeza mnyororo wa thamani wa zao la Mpunga na kutunza mazingira.
Mratibu wa Mradi huo kutoka Shirika la maendeleo la umoja wa Mataifa UNIDO Faustine Msangila ameyasema hayo katika Semina iliyowakutanisha wamiliki na Wawakilishi wa viwanda vya kuchakata mpunga katika eneo la Halmashauri ya mji wa Ifakara semina mbayo imefanyika hii leo Agosti 11,2025 katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo Ifakara.
Bwana msangila amesema katika Mradi huo wanashirikiana na Shirika la Kuhudumia viwanda vidogo (SIDO),chuo cha Nelson Mandela ambapo wanatarajia kuona watanzania wanamiliki uchumi wao kupitia Mnyororo wa thamani wa zao la mpunga kwa kuanza na viwanda vidogo wakitumia teknolojia rafiki kwa mazingira.

Akizindua warsha ya mradi huo mjini Ifakara, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya amesema kuwa wilaya hiyo ipo katika eneo la kimkakati, hivyo utekelezaji wa mradi huo umekuja mahali sahihi na kwa wakati mwafaka.
Wakili Kyobya amesema kuwa pamoja na Wilaya ya Kilombero kujikita katika uchumi wenye tija, pia imejielekeza katika uhifadhi wa mazingira hivyo, mradi wa kuzalisha mkaa mbadala utasaidia kupunguza uharibifu wa misitu kwa kutoa mbadala wa nishati ya kupikia kwa wananchi.
Amesema Mradi huo kufadhiliwa na Serikali ya Japan ni matokeo ya ushirikiano na mahusiano mazuri ya Rais Dkt.Samia na mataifa mbalimbali huku akitumia kikao hicho kutoa wito kwa taasisi za umma kuanza kutumia nishati mbadala ili kupunguza uharibifu katika maeneo yanayohifadhiwa kiasili.

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii Halmashauri ya Mji wa Ifakara Bi Florence Mwambene amesema ujio wa mradi huo unakwenda kuwa fursa kwa wakazi wa mji wa Ifakara na kwamba
Kupitia idara hiyo watakwenda kuhamasisha zaidi jamii kuinuka kiuchumi kupitia utengenezaji wa nishati hiyo safi ya kupikia.
Mradi huu wa mwaka mmoja unatekelezwa katika mikoa mitatu hapa Tanzania ambayo ni Mbeya,Shinyanga pamoja na Morogoro katika Mji wa Ifakara na unafadhiliwa na Serikali ya Japani ambao wanatamani jamii kuendea kiuchumi wakati huo mazingira yakibaki salama.