Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
15 July 2025, 2:25 pm

Lengo la mbio za hisani ni kutangaza utalii na kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kuhifadhi ILUMA
Na Katalina Liombechi
Katika kutangaza vivutio na kuendeleza bonde oevu la kilombero wadau na jamii inayounda hifadhi ya jamii ILUMA wanatarajia kufanya mbio za hisani kulinda eneo hilo muhimu kiikolojia.
Mbio hizo zinazojulikana kama ILUMA Half Marathon inatarajiwa kufanyika tarehe 30 Agosti mwaka huu, ambapo itatanguliwa na matukio mbalimbali ikiwemo kutolewa kwa elimu,michezo na kwamba mbio hizo zitahusisha wanariadha kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Mbali na mbio hizo, matukio mbalimbali ya kimichezo yanatarajiwa kufanyika, yakiwemo mashindano ya mpira wa miguu, michezo ya jadi, na burudani kutoka kwa wasanii wa ndani, ili kuhamasisha ushiriki wa jamii nzima.
Mashindano hayo ya nusu marathon yameandaliwa na Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii ILUMA, inayojumuisha vijiji 15 kutoka wilaya za Ulanga na Kilombero, mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa SUSTAIN ECO unaotekelezwa kwa ushirikiano wa AWF na IUCN.
Akizungumza na Radio Pambazuko FM Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, pamoja na Makamu wake, wamesema lengo kuu la tukio hilo nikutangaza vivutio vya kiutalii vilivyopo ndani ya maeneo ya jamiinakuelimisha juu ya umuhimu wa kuilinda hifadhi ya ILUMA WMA, ambayo ni sehemu muhimu ya bioanuwai katika bonde la Kilombero.
Mwenyekiti huyo wa jumuiaya ya hifadhi ya ILUMA amesema maandalizi yanakwenda vizuri huku akiwakaribisha wananchi, washirika wa maendeleo, na wadau wa uhifadhi kushiriki na kutoa mchango wao katika kuendeleza hifadhi ya jamii kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake Adam Kulanga makamu mwenyekiti wa hifadhi hiyo amezungumzia makundi yatakayoshiriki katika mchezo wa mpira wa miguu na zawadi zitakazotolewa.

Hifadhi ya jamii ILUMA yenye muunganiko wa Vijiji 15 inatokana na tarafa za Ifakara,Lupiro na Mang’ula zinazopatikana katika Wilaya za Ulanga na Kilombero Hifadhi hiyo ilianzishwa nov 21,2011 na ilipata haki ya matumizi ya rasilimali mei 5,2015 kwa Tangazo la serikali GN:102 ikiwa na ukubwa wa kilometa za Mraba 509,hivyo Mbio hizo za hisani ni kwa ajili ya kutoa elimu ya uhifadhi endelevu kwa maslahi mapana ya bonde la Kilombero.