Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
8 July 2025, 7:05 pm

Athari za mikopo isiyo rafiki hasa kwa wajasiriamali wadogo wengi hujikuta wakishindwa kulipa mikopo hiyo kwa wakati kutokana na viwango vya riba visivyodhibitika na hatimaye kudumaa zaidi kiuchumi
Na Katalina Liombechi
Imeelezwa kuwa Mikopo yenye riba kubwa maarufu kama chap chap imekuwa ikiwatesa wajasiriamali wadogo hali inayopelekea kuadhirika na wengine kukimbia na kutelekeza familia.
Baadhi ya wajasiliamali wadogo wananchi wa kitongoji cha uwanja wa ndege kata ya Kibaoni Tunu Kipendawazungu na Issa Siraji wameyasema hayo wakati wakizungumza na Pambazuko FM katika zoezi la kuwaandikisha wajasiliamali kwenye mfumo ili waweze kunufaika na mikopo kwa Wajasiliamali isiyo na riba ambayo inayotolewa na Serikali kupitia benki ya NMB.
Wananchi hao wamesema changamoto ya mikopo hiyo imekuwa ikifilisi watu na wakisalia kwenye hali duni hivyo ujio wa fursa ya mikopo hiyo itawakwamua zaidi kiuchumi.

Akizungumzia zoezi hilo na sifa za kunufaika na mikopo hiyo Afisa maendeleo ya jamii kata ya Kibaoni bi. Esther Mtweve amesema mikopo hiyo inayojulikana kama WBN imekuja wakati mwafaka na Serikali ya Dkt Samia imekusudia vyema kuwaondoa wananchi katika changamoto ya mikopo umiza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Bwana Jeremiah Machibya amesema hiyo ni fursa adhimu kwa wananchi wake huku akiwataka kujitokeza kwa wingi kusajiliwa na hatimaye kupata mikopo itakayowasaidia kukuza mitaji yao.

Zoezi la kuwasajili wajasiliamali wadogo kwenye mfumo linafanyika katika Wilaya nzima ya Kilombero na katika kitongoji cha Uwanja wa Ndege linafanyika katika shule ya Msingi Uwanja wa Ndege.