Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
5 July 2025, 9:38 am

“Klipu hiyo ni ya kutengenezwa yenye lengo la kunichafua hasa kipindi hiki cha mchakato wa uchaguzi ambacho kinakuwa na chuki na fitina zisizo za msingi kutoka kwa watu wenye nia mbaya ili nishindwe kusimamia uchaguzi wa kura za maoni kwa haki”
Na Katalina Liombechi
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilombero Ndugu Mohamed Msuya amekanusha vikali tuhuma zinazoenezwa mitandaoni kupitia klipu ya sauti inayomhusisha na madai ya kuhoji namna ya utaratibu wa wajumbe wa mkutano mkuu kutopewa nafasi ya kuuliza maswali kutoka maeneo wanayotoka kama inavyosikika sehemu ya sauti hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 4, 2025, katika ofisi za chama hicho zilizopo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara Msuya amesema klipu hiyo ni ya kutengenezwa na inalenga kumchafua hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa uchaguzi.
Amefafanua kuwa hajawahi kutoa kauli yoyote ya wajumbe kuzuiwa kuuliza maswali na kwamba lengo la kusambazwa kwa klipu hiyo ni kumharibia taswira yake mbele ya jamii na wanachama wa chama hicho.
Aidha, Msuya amesema tayari amechukua hatua kadhaa kuhusiana na tukio hilo ikiwemo kuripoti rasmi kwa jeshi la polisi huku akielezea imani yake kwa vyombo vya dola katika kushughulikia jambo hilo.
Msuya amesema Klipu hiyo iliyoanza kusambaa katika mitandao ya kijamii July 2,2025 ni ya uzushi huku akieleza kuwa kwa utaratibu wa Chama hicho mkutano mkuu unatoa nafasi kwa wajumbe kuuliza maswali na kupata majibu kutoka kwa Mwenyekiti wa chama Taifa Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo kwa upande wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilombero limekiri kuripotiwa kwa jambo hilo na kwamba wanaendelea na Uchunguzi.