Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
26 June 2025, 10:44 pm

Kwa eneo hili Ifakara wengi wamekwishalipa kodi tunaendelea kuwahimiza
Na Katalina Liombechi
Timu ya Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia Makao Makuu kwa kushirikiana na ofisi ya TRA mkoa wa Morogoro, imeendelea na ziara yake maalum katika mji wa Ifakara wilayani Kilombero, kwa lengo la kuwatembelea walipakodi, kusikiliza changamoto zao na kuwakumbusha umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.
Wakiwa Katika ziara hiyo leo, timu hiyo imebaini changamoto kadhaa zinazowakabili wafanyabiashara, kubwa ikiwa ni malalamiko kuhusu uelewa wa matumizi na matengenezo mashine za EFD pale zinapoharibika jambo ambalo limekuwa kero kwao kama navyoeleza mmoja wa wafanyabiashara Ifakara.
Kufuatia kero hiyo, timu hiyo ya TRA ilifika kwa wakala wa mashine za EFD, Bw. Jeremiah Machibya, kupata ufafanuzi juu ya suala hilo na kwamba Machibya ameeleza kuwa baadhi ya gharama hizo zinatokana na huduma na vipuri vinavyohitajika wakati wa matengenezo, huku akieleza muda mwingine wafanyabiashara wamekuwa wakitengeneza mazingira ya kujitetea.
Akizungumza katika ziara hiyo, Afisa Mwandamizi Msimamizi wa Kodi kutoka TRA mkoa wa Morogoro, Bi. Immaculate Chaggu, amesema kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wafanyabiashara wa Ifakara tayari wamelipa kodi zao, jambo linaloashiria uelewa na ushirikiano mkubwa kutoka kwa walipakodi.

Kwa upande wao, baadhi ya walipakodi waliozungumza na redio Pambazuko FM wamesema wamefurahishwa na huduma zinazotolewa na TRA kwa sasa, wakieleza kuwa ni rafiki zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Ziara hiyo iliyoanza Juni 23,2025 ambayo ni maelekezo ya Kamishina General wa Mamlaka hiyo ni sehemu ya mkakati wa TRA kuimarisha mahusiano na walipakodi, kutatua changamoto kwa haraka na kuhakikisha kila mfanyabiashara anatimiza wajibu wake wa kulipa kodi kwa hiari.