Pambazuko FM Radio

Tsh.Bil 6 kuleta mageuzi ya kiuchumi Mlimba

26 June 2025, 7:44 pm

Picha ya Wadau katika uzinduzi mradi wa FOLUR(Picha na Katalina Liombechi)

Mradi huu kuletwa Kilombero katika Halmashauri ya Mlimba unastahili kutokana na umuhimu wa bonde hili Kiuchumi na upekee wake kiikolojia

Na Katalina Liombechi/Kuruthumu Mkata

Mradi wenye thamani ya Tsh.Bil 6 wa Kuboresha Mifumo Jumuishi ya Usimamizi wa Chakula, Ardhi na Mazingira ya Asili unatarajiwa kuleta mafanikio makubwa Katika Halmashauri ya Mlimba Mkoani Morogoro.

Hafla ya utambuzi wa Mradi huo unaojulikana kama Forest Land use and Restoration(FOLUR) imefanyika Juni 25,2025 katika Ukumbi wa Mlimba uliopo Ifakara Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Katibu Tawala Wilaya ya Kilombero, Mheshimiwa Abraham Mwaikwila, ambaye alimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Mwaikwila amesema kuwa mradi huo ulistahili kuletwa wilayani Kilombero na ni wakati muafaka, hasa ikizingatiwa umuhimu wa Bonde hilo katika masuala ya kiikolojia na kiuchumi.

Sauti ya DAS Kilombero

Joseph Mgana Mratibu wa mradi huu alieleza kuwa mradi huo utakaotekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na utahusisha jamii moja kwa moja ili kuhakikisha kuwa matokeo yanakuwa ya kudumu kufanya kilimo endelevu cha zao la Mpunga usimamizi wa vyanzo vya maji na Usimamizi wa matumizi bora ya ardhi itakayosaidia kupunguza Migogoro kati ya hifadhi na maeneo ya wananchi.

Picha ya Joseph Mgana Mratibu Mradi FOLUR Mlimba(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Joseph Mgana Mratibu Mradi FOLUR

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Jamary Idrisa ameshukuru kwa mradi huo na kwamba watausimamia vizuri huku akitoa wito kwa wananchi wote wa Halmashauri ya Mlimba kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huo ili kufanikisha lengo kuu la kuboresha maisha kupitia matumizi bora ya rasilimali za chakula, ardhi na mazingira.

Sauti ya DED Mlimba

Wanjala Mgaywa ni Mratibu mkuu Mtekelezaji wa Mradi huo Kitaifa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii amesema jumla kuu ya Mradi huo wa Miaka mitano unagharimu kiasi cha Tsh.Bil 18 na kwa Tanzania unatekelezwa katika Halmashauri mbili huko zanzibar na kwa Tanzania Bara ni Halmashauri ya Mlimba pekee ikiwa ni maeneo hayo ni yenye mahitaji kulingana na hali ya kimazingira unafadhiliwa na mfuko wa Mazingira Duniani kwamba unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika usimamizi wa ardhi na rasilimali za asili na hatimaye kuwa mfano kwa maeneo mengine nchini.

Sauti ya Mratibu Mradi Kitaifa