Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
23 June 2025, 8:24 pm

Ulipaji wa kodi siyo tu wajibu wa kisheria, bali ni jukumu la kizalendo katika kuchangia maendeleo ya nchi
Na Katalina Liombechi
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Morogoro imeendelea kuwatembelea walipakodi kwa lengo la kuwakumbusha kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati, sambamba na kuhimiza ukadiriwaji wa kodi mapema kabla ya mwisho wa mwaka wa serikali.
Akizungumza hii leo leo Juni 23, 2025, katika ziara hiyo kwenye eneo la Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Afisa kutoka TRA mkoa wa Morogoro, Bi Emmaculatha Chagu, amesema ziara hiyo inalenga kuwakumbusha wananchi juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari ili kuiwezesha serikali kutoa huduma bora kwa jamii.
Bi Chagu ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za TRA kuimarisha mahusiano na walipakodi kwa njia ya uelewa na mawasiliano ya karibu.

Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara wameeleza kuridhika na huduma wanazozipata kutoka mamlaka hiyo na kwamba hawana sababu ya kukwepa kulipa kodi.
