Pambazuko FM Radio

TANESCO Moro yabaini hujuma miundombinu ya umeme

19 June 2025, 8:19 pm

Picha Ikionyesha Moja ya Miundombinu ya Umeme katika mtaa wa Magengeni Ifakara(Picha na Katalina Liombechi)

Katika kuendelea kutoa huduma iliyo bora ya umeme Shirika la TANESCO limebaini changamoto ya kuhujumu miundombinu ya  umeme kwa makusudi au kwa bahati mbaya

Na Katalina Liombechi

Shirika la Umeme Tanzania—TANESCO Mkoa wa Morogoro limebaini kuwepo kwa changamoto kubwa ya hujuma dhidi ya miundombinu ya umeme, hususan nguzo na nyaya, hali inayochochewa na biashara haramu ya vyuma chakavu pamoja na ukulima kwa kuchoma moto mashamba.

Akizungumza na Radio Pambazuko FM hii leo Juni 19,2025 wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Usalama wa miundombinu ya TANESCO Afisa Usalama wa Shirika hilo John Lugwecha  amesema kuwa vitendo hivyo vinaathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma bora na endelevu ya umeme nchini.

Afisa huyo ameeleza kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakihujumu miundombinu ya shirika hilo kwa kuvuna vyuma vya nguzo, kuchoma maeneo ya mashamba karibu na laini za umeme, au kufanya shughuli za kilimo bila kuzingatia tahadhari, jambo linalosababisha hitilafu za mara kwa mara.

Picha ya John Lugwecha Afisa usalama miundombinu ya TANESCO(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya John Lugwecha Afisa usalama miundombinu ya TANESCO

Tusa Mwakyusa Afisa Uhusiano na wateja wa shirika hilo Morogoro kusini (Ifakara) shirika hilo limewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za waharibifu wa miundombinu hiyo na kuzingatia usalama wakati wa shughuli zao ili kuhakikisha huduma ya umeme inabakia kuwa ya kuaminika na ya uhakika.

Picha ya Tusa Mwakyusa Afisa Uhusiano na wateja wa shirika hilo Morogoro kusini(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Tusa Mwakyusa Afisa Uhusiano na wateja wa shirika hilo Morogoro kusini

Aidha Afisa Usalama wa Shirika hilo John Lugwecha ameelezea mikakati na hatua zinazochukuliwa kwa wanaohujumu miundombinu ya Umeme ikiwa ni pamoja na kukutana na wauza vyuma chakavu na wadau kufuata utaratibu wa shughuli hiyo,kutoa elimu na wajibu,kuchukua hatua za kisheria na kushirikisha jamii kwa kutoa zawadi kwa watoa taarifa kuhusu uhujumu unaofanyika katika maeneo yao.

Sauti ya Afisa Usalama wa Shirika hilo John Lugwecha

Naye Kelvin Kasambala Afisa uhusiano na Wateja Morogoro Kaskazini ameikumbusha jamiikulipa madeni ya huduma hiyo kwa wakati ili waweze kuhudumiwa inavyostahili.

Picha ya Kelvin Kasambala Afisa uhusiano na Wateja Morogoro Kaskazini(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Kelvin Kasambala Afisa uhusiano na Wateja Morogoro Kaskazini

Mmoja kati ya Wafanyabiashara ya Vyuma chakavu Ifakara Joseph Johnson amesema yuko tayari kutoa ushirikiano kwa watu watakaopeleka vyuma vitokanavyo na miundombinu ya umeme.

Sauti ya Joseph Johnson mfanyabiashara vyuma chakavu Ifakara

Wiki ya usalama imezinduliwa chini ya kaulimbiu: “Lipa Deni, Linda Miundombinu, Tukuhudumie – Huduma Endelevu Inaanza na Wewe”, ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu wajibu wao katika kulinda miundombinu ya umeme pamoja na kulipa madeni kwa wakati.