Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
16 June 2025, 8:24 pm

“Lengo kubwa ni kumlinda mtoto aweze kutimiza ndoto zake,tunataka kila mtoto asome“
Na Katalina Liombechi
Wazazi na Jamii Wilayani Kilombero wametakiwa kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili watoto kama vitendo vya ukatili na wazazi kutoa ushirikiano katika malezi na lishe ili waweze kutimiza ndoto zao.
Haya yanakuja baada ya Watoto kuwasilisha changamoto zao kupitia risala yao katika Maadhimisho ya Mtoto wa Afrika ambapo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara Maadhimisho hayo kwa mwaka 2025 yamefanyika katika shule ya Msingi Kiningina, yakihudhuriwa na mamia ya wanafunzi, walimu, wazazi na wadau wa maendeleo ya watoto.
Katika risala hiyo iliyosomwa na wanafunzi Shaban Hassan na Rachel Ngalawa kwa niaba ya watoto wenzao wameeleza changamoto mbalimbali zinazowakumba ikiwa ni pamoja na ukosefu wa baadhi ya huduma muhimu, vitendo vya ukatili majumbani na kwenye jamii ambazo wamesema zinakwamisha maendeleo yao ya elimu.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, ambaye ametoa wito kwa jamii kuhakikisha watoto wanalelewa kwa upendo, ulinzi na kupata huduma zote muhimu, ikiwemo elimu, afya na chakula.
Aidha ameahidi kufuatilia kwa karibu masuala yote yaliyowasilishwa na watoto hao, huku akitoa maelekezo kwa idara zinazohusika kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa haraka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Bi Florence Mwambene, alisema kuwa ofisi yake imepokea kwa uzito mkubwa maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya, na kueleza kuwa utekelezaji wake unahitaji ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau mbalimbali.

Baadhi ya Wazazi waliohudhuria katika maadhimisho hayo pamoja naye Mwalimu Avit Mosha kutoka Shule ya sekondari Kilombero wamekiri kuwepo kwa changamoto zinazokwamisha maendeleo yao na kwamba wako tayari kuzifanyia kazi.

Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka tarehe 16 Juni kwa lengo la kukumbuka mauaji ya kikatili ya watoto waliokuwa wakidai haki yao ya elimu nchini Afrika Kusini mwaka 1976, na kuchochea juhudi za kutetea na kulinda haki za watoto kote barani Afrika ambapo mwaka huu 2025 kauli mbiu inasema “Haki ya Mtoto:tulipotoka,tulipo na tuendako”