Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
13 June 2025, 3:13 pm

Choo safi na salama husaidia kuzuia kuenea kwa magonjwa ya Mlipuko kama kipindupindu, kuhara, na minyoo hukinga uchafuzi wa mazingira unaoweza kusababishwa na kinyesi kuwa wazi au kutupwa hovyo
Na Katalina Liombechi
Halmashauri ya Mji wa Ifakara imeanza kuchukua hatua ya ukarabati wa Choo cha Stendi ya Kwa Makali baada ya Choo hicho kufungwa kwa Siku 5 na uongozi wa Stendi kutokana na hitilafu ya miundombinu.
Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti taka katika Halmashauri hiyo Bw.Gabriel Malisa akizungumza na Pambazuko FM hii leo June 13,2025 amesema utekelezaji wa kukarabati choo hicho ni sehemu ya majukumu yao kwani ilikuwa kwenye bajeti yao na kwamba baada ya wiki moja ukarabati utakuwa umekamilika.

Mhandisi wa Halmashauri hiyo Eng.Kelvin Eliah White akiwa katika eneo la ujenzi wa choo hicho amesema ukarabati huo umeanza June 12,2025 na Wanatarajia kumaliza June 18,2025 huku akieleza ukarabati huo unahusisha Kukarabati jengo la choo,miundombinu ya maji na mfumo wa maji taka ambapo baada ya siku chache wafanyabiashara wa eneo la stendi wataendelea kupata huduma ya choo kama ilivyokuwa awali.

Mwenyekiti wa Mtaa huo Deogratius Mwisongo na baadhi ya wafanyabiashara wameelezea kufurahishwa na kupongeza kwa hatua hiyo nzuri iliyochukuliwa na Ofisi ya Mkurugenzi ambayo itasaidia kuwafanya kuwa salama dhidi ya athari za kiafya wanapotumia huduma ya choo wanapokuwa katika eneo la Stendi.

Utakumbuka June 7,2025 Viongozi wa Stendi ya kwa makali na wafanyabiashara wa eneo hilo walichukua uamuzi wa kufunga choo cha Stendi hiyo wakihofia kukumbwa na magonjwa ya Mlipuko kufuatia miundombinu kuharibika na kupelekea kinyesi kuwa wazi.