Pambazuko FM Radio

Uongozi stendi Ifakara wafunga huduma ya choo

7 June 2025, 6:33 pm

Picha ya eneo la choo cha Stendi ya kwa makali ikionyesha maji taka(Picha na Katalina Liombechi)

Stendi hii inahudumia zaidi ya watu 400 kwa siku kwa sasa tunalazimika kuomba huduma za choo katika nyumba za jirani kitu ambacho si ustaarabu na inaleta usumbufu

Na Katalina Liombechi

Viongozi wa Stendi ya kwa makali iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara ambayo mabasi husafirisha abiria ndani na Wilaya jirani hii leo Juni 7,2025 wamelazimika kuchukua hatua ya kufunga huduma ya choo katika Stendi hiyo kutokana na mabomba kupasuka na kusababisha kinyesi kutapakaa hali inayozua taharuki miongoni mwa abiria na wafanyabiashara wa Stendi.

Kwa mujibu wa Viongozi na wafanyabiashara katika Stendi hiyo Renifrid Uhenge na Bushiri Goma wamesema hatua hiyo imefikiwa kwa lengo la kulinda afya za watumiaji wa Stendi kutokana na hali duni ya usafi iliyosababishwa na hitilafu hiyo na kupelekea maji taka kuzagaa katika eneo hilo.

Aidha choo hicho pia kinakabiliwa na ukosefu wa miundombinu bora ya maji na umeme jambo linalozidisha changamoto ya namna ya kupata huduma ya choo huku wakitishia kutokuwajibika kulipa ushuru mpaka wahakikishiwe huduma hiyo muhimu.

Picha ya Renifrid Uhenge Mwenyekiti Stendi kwa Makali(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti za viongozi wa Stendi kwa Makali

Mfanyabiashara wa chakula katika Stendi hiyo Rehema Waziri kutokana na hali hiyo ameelezea wasiwasi wa magonjwa ya mlipuko kwao binafsi na kwa wateja wanaowahudumia,huku anayefanya usafi katika choo hicho Ally Machemba akiomba kuboreshewa mazingira anayofanyia kazi kutokana na kujikuta yupo katika hatari zaidi kiafya.

Picha ya Rehema Waziri Mfanyabiashara ya chakula Stendi kwa Makali(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti za Mama lishe na Mfanya usafi choo cha Stendi kwa Makali

Mwenyekiti wa Mtaa wa Miembeni ilipo stendi ya kwa Makali Kata ya Ifakara Bwana Deogratius Mwisongo amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kwamba alichukuwa hatua ya kuiwasilisha kupitia vikao vya kamati ya maendeleo ya kata huku akiomba hatua za haraka kuchukuliwa kuepuka hatari inayoweza kujitokeza.

Picha ya Deogratius Mwisongo Mwenyekiti mtaa wa Miembeni ilipo Stendi(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Deogratius Mwisongo Mwenyekiti Mtaa wa Miembeni

Jitihada za kumtafuta Afisa afya wa Halamshauri ya Mji wa Ifakara zinaendelea ili kupata ufafanuzi wa jambo hilo na hatua zinazochukuliwa.