Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
31 May 2025, 10:35 am

Bonde la Kilombero ni maarufu kwa shughuli za kilimo na ni eneo muhimu Kiikolojia hivyo AGCOT wanaendeleza kilimo cha Kibiashara kinachotunza na kuhifadhi mazingira
Na Katalina Liombechi
Taasisi ya Kuendeleza Shoroba za Kilimo Tanzania AGCOT kupitia kwa Meneja wake Mkoa wa Morogoro John Banga amesema lazima kuwe na jitihada za pamoja kudhibiti shughuli za kiuchumi kwa kujali Mazingira.
John Banga ameyasema hayo wakati akizungumza na Radio Pambazuko FM kueleza juu ya tija na Umuhimu wa Kiikolojia wa Bonde la Kilombero lenye vyanzo vingi vya maji na viumbe hai adimu Duniani.
Haya yanakuja wakati huu Dunia ikikabiliwa na Mabadiliko ya tabianchi hali inayochochewa na Ukataji wa miti hovyo,makazi ndani ya maeneo ya hifadhi,uharibifu wa kingo za mito,uchimbaji wa Mchanga,utupaji holela wa vifungashio vya madawa ya kilimo mara baada ya matumizi hali ambayo amesema inatishia usalama wa bonde hilo.

Meneja huyo wa AGCOT Mkoa wa Morogoro amesema hatua muhimu za kuchukuliwa katika kuleta uendelevu wa Bonde la Kilombero ni kuwa na mikakati ya pamoja Miongoni mwa Wadau,wananchi na serikali ni pamoja na kukuza kilimo hifadhi kwa kuhamasisha mazao ya Kimkakati kama Karafuu Kokoa na mengineyo,kuainisha mipaka na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya ardhi na vyanzo vya maji,kuendeleza kampeni ya utunzaji wa miti SOMA NA MTI,ISHI NA MTI ambapo ili kufanikiwa zaidi wamekuwa wakishirikisha jamii hasa wanawake na vijana.
Akizungumzia kuelekea Siku ya Mazingira Duniani yatakayofanyika June 5 2025 Banga amesema kauli mbiu ya Mwaka huu inakumbusha udhibiti wa taka za plastiki haza za mashambani kuzihifadhi katika vizimba na baadaye kutoa taarifa kwa Idara za mazingira na kwa wadau ili zichukuliwe kwa usalama kwenda kuzirejereza ili kuzuia kuharibu mifumo ikolojia ya bonde la Kilombero.

“Tumechukua jukumu la pamoja kwenda kwa wakulima kupitia vikundi vyao kuwaelemisha juu ya kudhibiti taka za plasiki“
Ikumbukwe kuwa kauli mbiu ya siku ya mazingira kwa mwaka huu 2025 hapa Tanzania inasema ”Mazingira yetu na Tanzania ijayo tuwajibike, dhibiti matumizi ya plastiki”ikihamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na kuchukua hatua za kupunguza uchafuzi wa plastiki katika Halmashauri ya mji wa Ifakara maadhimisho hayo yatafanyika kata ya Ifakara na Kitaifa yanatarajiwa kufanyika jijini Dodoma mgeni rasmi anatarajia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.