Pambazuko FM Radio

Wakazi wa Viwanjasitini wapanda miti 2,000 kando ya mto Lumemo

24 May 2025, 1:57 pm

Picha ya baadhi ya wakazi wa Viwanjasitini wakipanda miti (Picha kwa hisani ya ofisi ya kata)

Kupanda miti katika eneo hilo ni jitihada za kuhakikisha kuwa Mto Lumemo unasalia kuwa chanzo safi na salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Na Katalina Liombechi

Katika jitihada za kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji wananchi wa Kata ya Viwanjasitini leo wamepanda miti 2,000 katika eneo la Mtaa wa Minarani kando ya Mto Lumemo.

Akizungumza katika zoezi hilo leo Mei 24,2025 Mtendaji wa Kata hiyo, Bi Hawa Ndachuwa amesema kuwa lengo kuu ni kuhifadhi chanzo hicho muhimu cha maji na kuimarisha hali ya mazingira katika eneo hilo.

Picha ya Bi.Hawa Ndachuwa Afisa Mtendaji kata ya Viwanjasitini (Picha kwa hisani ya ofisi ya Mtendaji)

Mbali na zoezi la upandaji miti, Afisa Mtendaji huyo pia alitumia mkusanyiko huo kuwakumbusha wazazi na walezi kuhusu wajibu wao wa malezi bora kwa watoto, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama na ulinzi wa watoto katika jamii.

Licha ya ‘ubize’ na shughuli za kujitafutia kipato tusisahau jukumu la malezi ya watoto wetu.

Wananchi walioshiriki waliipongeza ofisi ya kata kwa jitihada hizo, wakiahidi kuendeleza utunzaji wa miti iliyopandwa na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kimazingira.

Picha ya wananchi wa Viwanjasitini wakipanda miti(Picha kwa hisani ya Ofisi ya Kata)