Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
8 May 2025, 7:38 am
Na Katalina Liombechi

Wananchi wa Kijiji cha Kibaoni Halmashauri ya Mji wa Ifakara wametakiwa kutojichukulia sheria mkononi dhidi ya Bw. Thabiti Kapaulana anayedaiwa kufanya uharibifu wa mpunga uliopandwa na wanakijiji katika eneo la wazi la kijiji hicho kitongoji cha Stesheni kwa ajili ya lishe kwa watoto na watu wasiojiweza.
Haya yanakuja baada ya kile kilichoelezwa na wananchi hao katika mkutano wa hadhara ambao umefanyika Mei 7, 2025 uliohudhuriwa pia na Mkuu wa Kituo cha Polisi Ifakara SP Joseph Nzelantuzu.
Katika Kikao hicho wananchi akiwemo Kandele, Twaha Likaya, Rashid Namtuka Beno Rotali na Waziri Mtilaki wamesema Mnamo Mei 5, 2025 Thabiti Kapaulana aling’oa mpunga huo uliopandwa na wanakijiji na kuwauzia watu akidai kuwa eneo hilo ni lake jambo ambalo liliibua hisia za watu kutaka kujichukulia maamuzi yasiyofaa hali iliyopelekea jeshi la polisi kufika na kumchukua kwa ajili ya usalama wake licha ya mambo mengine na tabia zisizoipendeza jamii hiyo ambayo inadaiwa Bwana Kapaulana amekuwa akizifanya mara kwa mara kama kuanzisha migogoro,lugha za matusi na na kuharibu mali za kijiji wananchi waeleza kuchoshwa na tabia hizo.

Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Kituo cha Polisi Ifakara SP Joseph Nzelantuzu amekemea nia isiyo njema ya wananchi kutaka kujichukulia sheria mkononi ambapo ameitaka ofisi ya kijiji kufuata sheria kwa kuhakikisha tathimini inafanyika na kufungua kesi dhidi ya Thabiti Kapaulana huku akiwataka kuwa watulivu wakati haki inapokwenda kutendeka.
