Pambazuko FM Radio

IRAD yakabidhi miche 5,000 ya mikarafuu Kilombero

19 March 2025, 3:46 pm

“Wilaya ya Kilombero inatakiwa kuachana na kilimo cha mazoea chenye tija ndogo na kuelekeza nguvu kwenye mazao ya kimkakati kama vile mchikichi, karafuu, pamba, parachichi, kokoa na mengineyo.”-Dc Kilombero Wakili Dunstan Kyobya

Na Elias Maganga

Taasisi ya International Rainforest Agriculture Development Limited (IRAD) imetoa miche 5,000 ya mikarafuu kwa wakulima wa Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhamasisha kilimo cha mazao ya viungo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya miche hiyo yaliyofanyika nje ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Afisa Utafiti kutoka IRAD, Bw. Godfrey Kikula amesema hatua hiyo inalenga kuwahamasisha wakulima kuwekeza kwenye kilimo cha karafuu ili kuongeza kipato na kukuza uchumi wa eneo hilo.

Afisa Utafiti kutoka IRAD, Bw. Godfrey Kikula wa pili kutoka kushoto (Picha na Elias Maganga)

Sauti ya Afisa Utafiti kutoka IRAD, Bw. Godfrey Kikula

Akizungumza baada ya kupokea miche hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya aliishukuru IRAD kwa mchango huo mkubwa na kueleza kuwa miche hiyo itagawiwa kwenye halmashauri mbili za Ifakara na Mlimba.

Wakili Kyobya ameelekeza wakurugenzi, maafisa kilimo na maafisa elimu kuhakikisha miche hiyo inagawiwa kwa vikundi vya wakulima wakiwemo vijana na wanawake wajane pamoja na kupandwa kwenye maeneo ya shule kwa ajili ya elimu endelevu ya kilimo cha viungo.

Ameongeza kuwa wilaya ya Kilombero inatakiwa kuachana na kilimo cha mazoea chenye tija ndogo na kuelekeza nguvu kwenye mazao ya kimkakati kama vile mchikichi, karafuu, pamba, parachichi, kokoa na mengineyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya aliyevaa shati jeupe lenye madoa madoa(Picha na Elias Maganga)
Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya

Kwa upande wake, Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Dkt. Yuda Mgeni amesema watahakikisha miche hiyo inatunzwa na kugawiwa kwa vikundi maalum, hasa vijana, ili kuwasaidia kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo cha karafuu.

Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Dkt. Yuda Mgeni wa pili kutoka kulia(Picha na Elias Maganga)
Sauti ya Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Dkt. Yuda Mgeni