Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
3 February 2025, 7:41 pm
Na Katalina Liombechi

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA imesema itaendelea kushirikiana na wadau kushughulikia changamoto za kimawasilino ili kuhakikisha huduma hiyo inakuwa salama kwa watumiaji.
Meneja kitengo cha watumia huduma ya mawasiliano TCRA Mhandisi Kadaya Baluhye ameyasema hayo February 2,2025 katika Mafunzo kuhusu masuala ya Usalama wa Kimtandao kuwajengea uwezo Madiwani,Watendaji,wenyeviti,Viongozi wa CCM katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara Mafunzo ambayo yameandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Kilombero Mh.Abubakary Asenga na kufanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mlimba uliopo Ifakara.
Akiwasilisha Mada kwa viongozi hao Meneja huyo amesema Mamlaka hiyo imeanzisha dawati la kushughulikia changamoto za kimawasilino kwa kutoa elimu,kutatua Migogoro kati ya watoa huduma na watumia huduma ambapo ametumia fursa hiyo kuitaka jamii kuwa makini kwa kupunguza ukarimu katika mitandao kwa kutofuata maelekezo pasipo kujiridhisha,kutokuwa na haraka kulipia huduma mbalimbali,kuacha tamaa za kunufaika pasi kugharamia ili kufanya huduma ya mawasiliano kuwa salama.

Mkuu wa wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya Mgeni rasmi na OCD Mrakibu wa Polisi Wilaya ya Kilombero David Nkuba wamesema Uwepo wa TCRA ulete tija kwa jamii kukabiliana na Wizi wa Mtandaoni kuhakikisha hakuna anayenufaika na shughuli hiyo ambayo inaichafua Wilaya ya Kilombero.
Mbunge wa Jimbo hilo Mh.Abubakary amesema ameamua kuandaa semina hiyo ili kuokoa kundi la vijana ambao ndio wamekuwa wakijihusisha na wizi huo ambao imekuwa aibu na hatari kwa uendelevu wa vijana wanaotarajiwa kujenga Taifa la Tanzania.
