Wakulima halmashauri ya mji Ifakara walia na geti la Idete
3 June 2024, 9:06 pm
Wakulima wa halmashauri ya mji wa Ifakara wengi wao wanalima mbali na makazi yao, ambapo baada ya mavuno hulazimika kurudisha mazao nyumbani, hapo ndipo hukumbana na kikwazo cha kulipia ushuru mazao hayo.
Na Isidory Matandula
Wakulima katika halmashauri ya mji Ifakara wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro wamemlalamikia Mkuu wa Wilaya ya Kilombero wakili Dunstan Kyobya suala la kutozwa ushuru katika geti la Idete ilhali mazao wanayopitisha si kwa ajili ya biashara. Malalamiko hayo yametolewa Jumamosi katika ofisi ya afisa mtendaji kata Viwanja Sitini mjini Ifakara baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo kuruhusu wananchi kutoa kero zao
Akijibu kero ya geti la Idete, Mkuu wa Wilaya huyo wakili Dunstan Kyobya amesema wakulima wanatakiwa kujisajili katika maeneo wanayolima ili waweze kuwabaini wafanayabiashara ambao ndio wanatakiwa kulipa ushuru katika vizuizi hivyo.
mkuu wa wilaya ya Kilombero wakili D. Kyobya – picha na; Isidory Matandula
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kilombero Abubakari Asenga amesema mkulima wa ndani ya wilaya ambaye haendi kuuza anayebeba mazao chini ya tani moja hapaswi kulipia ushuru kwani matumizi ya mazao hayo ni kwa ajili ya chakula na si vinginevyo.
Mbunge Abubakari Asenga akiongea na wananchi wa kata ya Viwanja sitini mjini Ifakara. picha na; Isidory Matandula
Sauti ya mbunge Asenga
Mkutano huo ulikuwa na lengo la kugawa msaada kwa waathirika wa mafuriko wa kata ya Viwanja Sitini mjini Ifakara wapatao 349 uliotolewa na shirika la Plan International Unit ya Ifakara kwa msaada wa Start Network mtandao wa kusaidia maafa kwa ushirikiano na taasisi kadhaa kutoka Umoja wa Ulaya.