Uharibifu wa mazingira unavyogharimu maisha ya watu
28 March 2024, 5:13 pm
‘‘Mnapojadiliana mikakati mtakayokuja nayo ni lazima, lazima nasema lazima ijibu hali ya umasikini sio kumwambia mtu asikate mti bila kumwambia afanye nini’’ Amesema Katibu Tawala Alhaj Mussa Ally Mussa
Na Katalina Liombechi
Imeelezwa kuwa Matokeo ya Uharibifu wa Mazingira katika Sehemu moja yanagharimu Maisha ya Watu Nchi nzima na Dunia kwa Ujumla.
Hayo yamebainika katika Warsha ya Siku tatu iliyowakutanisha Wadau wa Mazingira kutoka Katika Wilaya ya Kilosa,Mlimba na Mji wa Ifakara kujadili na Kupata Masuluhisho ya Asili(NATURE BASED SOLUTIONS)Katika Bonde la Kilombero Kikao ambacho kimefanyika katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara Ukumbi wa TTCIH na Kuja na Mikakati ya Kukabiliana na Changamoto zitokanazo na Shughuli za Kibinadamu ambazo zinahatarisha uendelevu wa Rasilimali Mbalimbali.
Awali Mgeni Rasmi Katika Warsha hiyo Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Alhaj Mussa Ally Mussa wakati akizindua kikao hicho March 25, 2024 aliwasisitiza Wadau hao kujadiliana na kuja na Mikakati itakayojibu hali ya Umasikini kwa Wananchi huku uasili ukiendelezwa.
Meneja wa Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori Afrika(AWF)Clarence Msafiri akizungumza wakati wa Majumuisho wa Kikao kazi hicho amesema Lengo la Kuwakutanisha wadau hao ni kuja na Mkakati wa Pamoja ili kuepusha kukinzana kwa namna ya Utekelezaji wa Miradi mbalimbali katika Sehemu zao za Kazi.
Amesema Kwa sasa Dunia inashuhudia Mabadiliko ya Tabia Nchi ambayo huenda yamesababishwa na Sehemu Moja,hivyo Mikakati iliyowekwa na Wataalamu hao anaamini itakuwa na Matokeo chanya kama itatekelezwa kwa kuzingatia uasili wa Eneo husika na kutatua changamoto za kiuchumi zinazoikumba jamii kwa kuwaelimisha,kuhamasisha,kuwapa njia Mbadala ya kujipatia Kipato na kurejesha uasili wa Maeneo yaliyoharibiwa
John Banga Meneja Uwanda wa Kilombero kutoka Taasisi ya Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) amesema kikao hicho kimekuwa na Matokea Mazuri kwani itawasaidia Wadau wa Mazingira kutekeleza mambo mbalimbali ya kurejesha Uasili katika maeneo wanayoyafanyia kazi pasipo kuathiri Mazingira na Uchumi wa Watu.
Baadhi ya Wadau walihudhuria warsha hiyo akiwemo Christina Kurunge kutoka KOCD ameelezea kufurahia Kushiriki kikao hicho ambacho kimeleta Mawazo ya pamoja Huku Mkulima wa Miwa Kutoka Tarafa ya Kidatu Abdi Mwimbi amesema imemsaidia kufahamu namna walivyokuwa wanaharibu Mazingira pasi Wao kujua kwa kutupa hovyo Makopo ya Madawa mara baada ya kutumia katika Mashamba yao hali ambayo inahatarisha usalama wa watu na viumbe wengine.
Warsha hiyo ambayo imefanyika Kuanzia March 25-27,2024 imeandaliwa na AWF kwa Kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira(IUCN)kupitia Mradi wa Miaka Mitatu wa SUSTAIN-ECO wanaoutekeleza kwa Pamoja kwa kushirikiana na Wadau Wengine wa Utunzaji wa Mazingira unaolenga Kurejesha Mifumo Ikolojia katika Wilaya ya Kilosa,Mlimba na Mji wa Ifakara Mradi ambao unafadhiliwa na Serikali ya SWEDEN.