Pambazuko FM Radio

Wananchi wagomea ujenzi wa kizimba cha taka-Ifakara

29 March 2023, 7:07 pm

Wananchi wa Mtaa wa viwanja sitini A wakiwa kwenye mkutano{Picha na Katalina Liombechi}

Wananchi wa Mtaa wa Viwanja Sitini A katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara wamegomea ujenzi wa kizimba cha taka kwenye eneo la makazi wakidai kuwa inaweza kuleta athari za kiafya

Na Katalina Liombechi

Wakazi wa Mtaa wa Viwanjasitini A katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara Wilayani Kilombero,wamegomea Ujenzi wa Kizimba cha taka katika eneo la wazi lililopo katika Mtaa huo wakihofia athali za Kiafya.

Hayo yamebainika katika Mkutano wa dharura wenye ajenda moja ya kujadili Ujenzi huo katika Mtaa huo mkutano ambao ilitakiwa awepo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Ndugu Lena Nkaya badala yake amemuagiza Afisa Afya wa Halmashauri  hiyo Bwana Jafari Ngogomela kufika na kutoa elimu juu ya Ujenzi wa Kizimba cha taka na Umuhimu wake.

Akitoa Elimu Hiyo Afisa Afya huyo Bwana Ngogomela amesema Kizimba ni eneo la makusanyo ya taka kwa muda mfupi ambapo ameeleza taka zinatakiwa kukaa ndani ya masaa 72 tu kutokana na kukua kwa mji huku akirejea Sheria ya Afya Halmashauri ya Eneo la Mji hairuhusiwi taka kuhifadhiwa majumbani kutokana na athali mbalimbali zinazoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na kuzalisha vijidudu vya Magonjwa.

Hata hivyo amesema uondoaji wa Taka hizo unategemea utaratibu wa uchangiaji wa fedha za Tozo.

Aidha amesema ujenzi wa Kizimba hicho ni kutokana na maagizo ya Mkuu wa Wilaya hiyo Wakili Dunstan Kyobya kuitaka Ofisi ya Mkurugenzi kuangalia eneo la kujengwa kizimba katika kata hiyo kutokana na kero iliyowasilishwa na baadhi ya wananchi wa Kata hiyo kukosekana kwa eneo la kutupa taka kwa muda kero ambayo iliwasilishwa katika mkutano alioufanyika katika Shule ya Msingi Jongo.

Afisa Afya wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Bwana Ngogomela {Picha na Katalina Liombechi}
Sauti ya Afisa Afya wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Bwana Ngogomela akitoa elimu ya umuhimu wa Kizimba

Wakizungumza katika Mkutano huo Baadhi ya Wananchi wa Mtaa huo akiwemo Hassan Mangauka,Janeth Likulu,Huba Mposindawa,Mussa Kaengo na Nuru kisweka wamesema hawafahamu kuhusu makubaliano ya ujenzi wa Kizimba katika eneo hilo huku wakielezea wasiwasi wao wa kukumbwa na magonjwa ya Mlipuko endapo ikitokea taka zitakaa katika Kizimba hicho kwa zaidi ya muda unaotakiwa huku wakitolea Mfano katika kizimba Kilichopo katika Soko kuu la Ifakara Mjini ambapo wameeleza licha ya kutokuwepo kwa changamoto ya kutolipwa fedha za Tozo,taka zimekuwa zikikaa kwa zaidi ya Siku sita mpaka saba.

Huba Mposindawa ni miongoni mwa wananchi waliohudhuria mkutano huo{Picha na Katalina Liombechi}
Sauti za wananchi wakigomea ujenzi wa Kizimba

Kufuatia hali hiyo imemlazimu Mwenyekiti wa Mtaa wa Viwanjasitini A,Bi Farida Kimbwembwe kuahirisha Mkutano huo kutokana na wananchi kukataa ujenzi wa Kizimba katika Eneo hilo.

CUE IN……MWENYEKITI.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Viwanjasitini A,Bi Farida Kimbwembwe{Picha na Katalina Liombechi}
Sauti ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Viwanjasitini A,Bi Farida Kimbwembwe akiahirisha mkutano