Boma Hai FM

Kifua kikuu kinatibika kwa matumizi sahihi ya dawa – Dkt Shirima

24 March 2026, 10:48

Pichani ni wananchi wa kata ya Machame Narumu waliojitokeza kupata elimu kuhusu ugonjwa wa Kifua kikuu(picha na Stanley Christian)

Kila ifikapo Machi 24,dunia huadhimisha siku ya kifua kikuu ,lengo ikiwa ni kuwakumbusha wananchi kuhusu ugonjwa huo, na kuwapatia elimu na kendelea kuchukua tahadhari.

Na Stanley Christian

Hai-Kilimanjaro

Katika kuelekea maadhimisho ya siku ya Kifua kikuu na Ukoma duniani wananchi wa Kijiji cha Usari kata ya Machame Narumu wilayani Hai  mkoani Kilimanjaro wamepatiwa elimu inayohusu utambuzi wa  dalili mbali mbali za ugonjwa huo,namna ya kujikinga  pamoja na tiba zake.

Akizungumza katika mafunzo hayo Machi 23, 2026 katika Zahanati ya Narumu mratibu wa Kifua kikuu na Ukoma wilaya ya  Hai Dkt Elirehema Shirima amesema kuwa maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka tarehe 24 Machi na kwa wilaya ya  Hai Maadhimisho ya Kifua kikuu yatafanyika katika vituo vyote vinavyotoa huduma  za afya.

Amesema  ugonjwa wa  kifua kikuu umekuwa  changamoto  kwa jamii hivyo lengo nikuwakumbusha wananchi kuchukua tahadhari kwani ugonjwa huo huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja Kwenda kwa mtu mwingine kwa kukohoa, kupiga chafya au kwa kuongea.

Aidha ametaja dalili kuu za ugonjwa huo kuwa ni kuwa na kikohozi kuanzia wiki mbili au zaidi na muda mwingine makohozi kuchanganyikana na damu,kupungua uzito pasipokua na sababu ya msingi,kutoka jasho jingi,pamoja  na homa za mara kwa mara wakati wa jioni.

Hata hivyo Dkt Shirima ametoa wito kwa wananchi wanapoona dalili hizo wajitokeze kwa haraka kufanya uchunguzi ili kupata matibabu mapema kwani ugonjwa wa Kifua kikuu unatibika kwa kutumia dawa kwa usahihi.

Sauti ya Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma wilaya ya Hai Dkt Elirehema Shirima

Nao wananchi wameshukuru kupata elimu hiyo na kwamba itawasaidia kujua dalili ili waweze kuchukua tahadhari mapema.

Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka  duniani Machi 24 na mwaka huu ikiwa na kauli mbiu isemayo  “Kwa jitihada za pamoja  za viongozi ,wadau na wananchi inawezekana kutokomeza kifua kikuu nchini”.