Boma Hai FM
Boma Hai FM
6 March 2026, 4:33 pm

Katika kuendelea kuboresha huduma za afya hapa nchini wadau wa maendeleo kutoka taasisi ya Tumbili Foundation kwa kushirikiana na Holcim Foundation kutoka nchini Switzerland wamejenga jengo la baba, mama na mtoto katika zahanati ya Nkweshoo na kulikabidhi kwa serikali.
Na Elizabeth Mafie &Salma Mgosso
Hai – Kilimanjaro
Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya elimu, afya na miundombinu ya barabara katika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha maisha ya wananchi ambapo wilaya ya Hai imepatiwa zaidi ya shilingi bilioni thelathini tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingia madarakani.


Hayo yamebainishwa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Hai Dionis Myinga, Machi 5, 2026 alipokuwa katika hafla ya kukabidhiwa jengo la baba, mama na mtoto katika zahanati ya Nkweshoo iliyopo kijiji cha Nkuu Ndoo kata ya Machame Mashariki.
Jengo hilo limejengwa na wadau wa maendeleo Tumbili Foundation kwa kushirikiana na Holcim Foundation kutoka nchini Switzerland, ambapo ujenzi wake umegharimu shilingi milioni mia moja arobaini.


Myinga amesema wafadhili wa mradi huo wamefanya kazi nzuri kwani mradi huo unagusa maisha ya wananchi moja kwa moja kwa kuboresha huduma za afya katika kata ya Machame Mashariki na kwamba wadau wengine wa maendeleo waendelee kujitokeza na kushirikiana na serikali kutekeleza miradi inayogusa maisha ya wananchi.
Akisoma taarifa ya mradi mwanzilishi wa Tumbili Foundation, Stephan Manimo, amesema taasisi hiyo itaendelea kusaidia na kuunga mkono miradi ya maendeleo nchini na kwamba taasisi hiyo ina utaratibu wa kipekee ambapo kila safari wanayoandaa huzalisha rasilimali zinazosaidia kutekeleza miradi yenye manufaa kwa jamii.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Machame Mashariki Jordan Ngowi, amewashukuru wadau hao wa maendeleo kwa kutekeleza mradi huo akisema kuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi wa eneo hilo ambao hapo awali walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Nao wananchi wa kijiji cha Nkweshoo katika kata ya Machame Mashariki wamesema kuwa ujenzi wa jengo hilo utawasaidia kupata huduma za afya karibu na kwa wakati.