Boma Hai FM
Boma Hai FM
5 March 2026, 9:10 am

Katika hafla ya kuwapongeza walimu wa kata ya Masama Magharibi iliyofanyika Machi 3, 2026 mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Omar Bomboko, amesisitiza umuhimu kuandaliwa kwa mpango kazi madhubuti wa kitaaluma ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, akitaja nidhamu, ubunifu na matumizi ya TEHAMA kuwa nguzo muhimu za elimu .
Na Elizabeth Mafie & Stanley Christian.
Hai-Kilimanjaro
Mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Omar Bomboko amewataka wataalamu wa elimu wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kuandaa mpango kazi madhubuti wa kitaaluma utakaosaidia kuimarisha ubora wa ufundishaji Ili kuendelea kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari za wilaya ya Hai.

Bomboko ametoa wito huo Machi 3, 2026 akiwa mgeni rasmi katika hafla ya kuwapongeza walimu wa Kata ya Masama Magharibi kwa matokeo mazuri ya kitaaluma, akisisitiza umuhimu wa nidhamu, ubunifu pamoja na matumizi sahihi ya TEHAMA ili kuendana na mabadiliko ya elimu ya kisasa.
Kwa upande wake afisa elimu wa Kata ya Masama Magharibi Raymond Mchome, amesema mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya walimu, wazazi na uongozi wa kata na kwamba juhudi zinaendelea kuboresha miundombinu ya shule na kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kufundishia pamoja na TEHAMA ili kuinua zaidi kiwango cha elimu na kamba mshikamano wa wadau wa elimu utaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya taaluma katika kata hiyo.

Nae diwani wa kata hiyo Eliufoo Happy Christopher, amesema uongozi wa kata unaendelea kuweka mikakati ya kutambua mahitaji ya shule na kuyafanyia kazi kwa hatua za muda mfupi na muda mrefu, kwa lengo la kudumisha na kuongeza mafanikio yaliyopo.
Hata hivyo waalimu waliopongezwa wameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia maadili ya taaluma na kutumia mbinu bunifu za ufundishaji ili kuimarisha zaidi matokeo ya wanafunzi na kudumisha heshima ya elimu katika Wilaya ya Hai.

Hafla hiyo imeandaliwa na Ofisi ya Diwani wa Kata ya Masama Magharibi kwa kushirikiana na Ofisi ya Afisa Elimu Kata, ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuthamini mchango wa walimu katika maendeleo ya elimu.
