Boma Hai FM

Migogoro katika familia yatajwa chanzo ukatili wa kijinsia

5 March 2026, 7:44 am

Picha kwa msaada wa mtandao.

Kutokana na migogoro mbalimbali katika baadhi ya familia hapa nchini ,migogoro hiyo imetajwa kuwa sababu kuu ya ukatili wa kijinsia.

Na Oliva Joel

Hai-Kilimanjaro

Migogoro baina ya wanandoa imetajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu zinazochochea vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia katika jamii, huku athari zake zikiendelea kuathiri ustawi wa familia na maendeleo ya watoto na kwamba  kunapokosekana maelewano, mawasiliano mazuri na ushirikiano ndani ya ndoa, hali hiyo inaweza kuibua migongano inayoweza kusababisha ukatili wa kimwili, kihisia na hata kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa marchi 1,2026 na Hapyness Eliufoo mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la GAESO lililopo wilayani Hai  mkoani Kilimanjaro linalojishughulisha na masuala ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia wakati  akizungumza na radio Boma Hai FM.

Amesema baadhi ya migogoro katika ndoa husababishwa na wanandoa kushindwa kuweka wazi vipato vyao, hali inayoweza kuleta migongano ya kifamilia pamoja  kutokuwepo kwa uwazi katika masuala ya kifedha kunachochea hali ya kutoaminiana na ubinafsi, jambo ambalo linaweza kuathiri ustawi wa familia kwa ujumla.

Aidha amebainisha kuwa tabia ya kuficha mali au mapato kunaweza  kuwasababishia watoto changamoto kubwa pale inapotokea kifo cha ghafla, kwani baadhi ya mali hubaki bila kutambulika rasmi na hivyo kuwanyima haki zao za msingi.

Sauti ya Hapyness Eliufoo mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la GAESO lililopo wilayani Hai  mkoani Kilimanjaro.

 Hata hivyo Eliufoo ameongeza kuwa wanawake wanapaswa kutambua kuwa dhana ya “hamsini kwa hamsini” inalenga katika fursa za kiuchumi na uwajibikaji huku akisisitiza  katika masuala ya kifamilia kunahitajika ushirikiano wa pande zote mbili, ambapo baba anapaswa kuwa kiongozi wa familia na mama kutekeleza wajibu wake ipasavyo, ili kujenga familia imara, yenye maelewano na malezi bora kwa watoto.