Boma Hai FM

Baraza la madiwani Hai lapitisha bajeti ya zaidi ya bilioni 52,vipaumbele vyatajwa

26 February 2026, 1:20 pm

Pichani ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka (katikati) pamoja na makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hai Trael Mboya (wa kwanza kulia)na Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Hai Dionis Myinga(picha na Praygod Munisi)

Baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro limepitisha bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni hamsini na mbili kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Na Elizabeth Mafie

Hai – Kilimanjaro

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya  ya Hai mkoa wa Kilimanjaro  Edmund Rutaraka, amesema baraza la madiwani limepitisha bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni 52 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, itakayolenga kuimarisha huduma za elimu, afya pamoja na miundombinu ya barabara katika wilaya ya Hai.

Bajeti hiyo imeidhinishwa  februari 25, 2026 katika kikao maalumu cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai, ambapo msisitizo umewekwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Pichani ni baadhi ya watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Hai wakifuatilia baraza la madiwani katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Hai(picha na Praygod Munisi)

Akiwasilisha mapendekezo ya mpango na bajeti kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Afisa Mipango na uratibu wa halmashauri, Saidi Abdalah amesema fedha hizo zitaelekezwa katika ujenzi na ukarabati wa shule, vituo vya afya pamoja na barabara za ndani ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Sauti ya afisa mipango na uratibu halmashauri ya wilaya ya Hai Said Abdalah.

Baadhi ya madiwani walichangia hoja mbalimbali wakisisitiza usimamizi makini wa miradi na matumizi sahihi ya fedha za umma ili kuhakikisha malengo yaliyopangwa yanafikiwa kwa ufanisi.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Gasper Ijiko amehimiza uwajibikaji na ushirikiano katika utekelezaji wa miradi hiyo, huku wananchi wakihimizwa kushiriki kikamilifu katika kulinda na kutunza miundombinu inayojengwa.

Pichani ni baadhi ya madiwani wakiwa katika baraza la madiwani ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Hai(picha na Praygod Munisi)

Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka amewataka madiwani na wataalamu kuongeza juhudi katika kusimamia miradi ya maendeleo ili bajeti iliyopitishwa iweze kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Sauti ya mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka.