Boma Hai FM

Makubaliano ya wazazi kuimarisha taaluma Hai Day Sekondari

30 January 2026, 1:15 pm

Pichani ni wazazi wa wanafunzi wanaosoma kidato cha pili na cha nne shule ya Sekondari Hai Day wakiwa katika kikao kilichofanyika katika shule hiyo(picha na Vivian Kweka)

Shule ya Sekondari Hai Day ni miongoni mwa shule za serikali zinazofanya vizuri kitaaluma kutokana na makubaliano ya wazazi kushiriki mchango wa chakula, kufuatilia kwa karibu maendeleo ya wanafunzi, kudhibiti utoro ,kushirikiana na walimu katika kuboresha mazingira ya kujifunzia ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi .

Na Vivian Kweka

Hai-Kilimanjaro

Imeelezwa kuwa jukwaa la wazazi katika Shule ya Sekondari Hai Day linaendelea kuweka mikakati mbalimbali itakayosaidia kukuza taaluma na kuleta maendeleo kwa wanafunzi, ikiwemo mchango wa chakula shuleni pamoja na ufuatiliaji wa maendeleo ya kielimu kwa wanafunzi.

Hayo yamebainishwa  Januari 29, 2026, katika kikao kilichofanyika shule ya sekondari Hai Day iliyopo wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro, kikihusisha wazazi wa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne ambao ni madarasa ya mitihani, kwa lengo la kuweka makubaliano ya pamoja yatakayosaidia kuboresha matokeo ya kitaaluma.

Katika kikao hicho, mwenyekiti wa jukwaa la wazazi wa shule hiyo, ndugu Samwel Mgonja, ameeleza kuwa ushiriki wa wazazi katika masuala ya chakula shuleni na ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo ya watoto wao ni nguzo muhimu katika kuhakikisha ufaulu mzuri.

Sauti ya mwenyekiti wa jukwaa la wazazi shule ya sekondari Hai Day Samwel Mgonja.

Aidha, imeelezwa kuwa kwa kushirikiana kwa karibu kati ya wazazi, walimu na uongozi wa shule, Shule ya Sekondari Hai Day itaendelea kufanya vizuri zaidi kitaaluma sambamba na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo mpango wa kuchimba kisima cha kuhifadhia maji kutokana na changamoto za miundombinu ya shule.

Pichani ni mkuu wa shule ya sekondari Hai Day Mwalimu Alex Warioba akizumgumza katika kikao hicho(picha na Vivian Kweka)

Kwa upande wake mzazi wa mwanafunzi anaesoma katika shule ya Sekondari Hai day Preygod Christian, amewahimiza wazazi kuwapa watoto wao muda wa kujisomea wanapokuwa nyumbani, kuepuka kuwabebesha majukumu mengi ya kazi na pia kuwapa nafasi ya kushiriki michezo mbalimbali itakayowasaidia kujenga uwezo wa kiakili na kimwili.

Naye mzazi mwingine, Charles Unjiro, ameipongeza Shule ya Sekondari Hai Day kwa kuandaa kikao hicho, akieleza kuwa shule hiyo inaendelea kufanya vizuri kitaaluma na imeimarisha ulinzi, hali inayochangia kuwepo kwa mazingira salama ya kujifunzia.

Pichani ni mwenyekiti wa jukwaa la wazazi shule ya sekondari Hai Day Samwel Mgonja akizungumza katika kikao hicho(picha na Vivian Kweka)