Boma Hai FM
Boma Hai FM
26 January 2026, 2:36 pm

Madiwani wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wamehimizwa kusimamia kwa karibu shughuli za serikali za mitaa ili kuhakikisha uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali za umma ,Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka, wakati akifunga mafunzo ya madiwani yaliyofanyika kwa siku mbili, huku akisisitiza usimamizi wa miradi na fedha za maendeleo.
Na Juma Robert Hai – Kilimanjaro
Madiwani wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuhakikisha wanasimamia vyema uendeshaji wa shughuli za serikali za mtaa katika halmashauri ya wilaya ya Hai ili kujenga halmashauri yenye hati safi kwa kipindi chote cha miaka mitano.

Hayo yameainishwa na mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka wakati akifunga rasmi mafunzo ya madiwani yaliyofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Halmashauri ya Hai.

Rutaraka amesema mafunzo hayo yatawasaidia madiwani kufahamu majukumu yao kikamilifu na namna ya kusimamia utekelezaji wake, ikiwa ni pamoja na kusimamia vyema fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi mbalimbali katika kata zao.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Masama Kusini Cedric Pangani, amesema mafunzo hayo yamekuwa chachu ya kujenga uelewa wa pamoja kuhusu nafasi ya madiwani katika kuimarisha demokrasia ya ndani na mahusiano bora na wananchi.
Amesema mafunzo hayo pia yanalenga kuwajulisha wananchi kuhusu uwajibikaji wa mabalozi wa mtaa, kwa kuhakikisha wananchi wanatoa taarifa za wageni wanaoingia kwenye mtaa ili kujulikana katika kaya husika na kuimarisha usalama wa wananchi wa mtaa au kata husika.