Boma Hai FM

Madiwani Hai wanolewa maadili na sheria

25 January 2026, 8:49 am

Pichani ni afisa utumishi mkoa wa Kilimanjaro Amosi Macharika akizungumza katika mafunzo kwa madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Hai (picha na Faraja Ulomy)

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai wamepewa mafunzo maalum ya siku mbili yaliyolenga kuwajengea uwezo katika utendaji kazi, hususan kuzingatia sheria, maadili ya uongozi na uwajibikaji. Mafunzo hayo yaliyofanyika Januari 23, 2026 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, yamelenga kuimarisha ufanisi wa madiwani na kuzuia migogoro kati yao na watendaji kwa maslahi ya wananchi.

Na Faraja Ulomy

Hai-Kilimanjaro

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro watakiwa  kutekeleza majukumu yao kwa weledi, kuzingatia sheria pamoja na kutambua stahiki zao kama haki ya msingi wanapokuwa kazini, ili kuepuka migongano na migogoro isiyo ya lazima katika utekelezaji wa majukumu yao.

Wito huo umetolewa na Afisa Utumishi wa Mkoa wa Kilimanjaro Amosi Machirika, akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdini Babu, wakati wa ufunguzi wa semina ya madiwani iliyofanyika Januari 23, 2026, katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Amosi Machirika amesema semina hiyo ya siku mbili imelenga kuwajengea uwezo madiwani katika utendaji kazi wao, hususan kwa kuzingatia sheria, taratibu na maadili ya uongozi.

Sauti ya afisa utumishi mkoa wa Kilimanjaro Amosi Macharika

Amesema kuwa miongoni mwa mada zitakazofundishwa ni utambuzi wa sheria, majukumu ya madiwani na namna bora ya utekelezaji wa kazi, ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika ngazi ya halmashauri.

Kwa upande wake afisa tawala  mkoa wa Kilimanjaro, Mashaka Juma, ambaye pia ni mtoa mada katika mafunzo hayo, amesema semina hiyo itachukua siku mbili na itahusisha mada 11, zikiwemo mada za maadili na uongozi kwa madiwani.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka amesema baraza la madiwani la awamu iliyopita lilikuwa na uadilifu mkubwa, hali iliyotokana na mafunzo waliyopewa, hususan katika usimamizi bora wa mapato na matumizi ya fedha.

Pichani ni baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Hai(picha na Faraja Ulomy)

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha madiwani wa sasa kuendelea kusimamia vyema majukumu yao kwa maslahi ya wananchi.

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo Diwani wa Kata ya Bomang’ombe Evodi Njau, amesema mafunzo hayo yamewajengea uelewa mpana katika utendaji kazi na kusaidia kuimarisha uwajibikaji wao.

Sauti ya Diwani kata ya Boman’gombe Evod Njau.

Aidha, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Hai, Manguba Maganda, amesema mafunzo hayo ni muhimu na amewataka madiwani kuyazingatia na kuyatumia katika utekelezaji wa majukumu yao  ya kila siku.

Pichani ni afisa utumishi mkoa wa kilimanjaro Amosi Macharika (wa nne kulia) mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Hai Wanguba Maganda( wa pili kulia) mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hai Edmund Rutaraka ( wa tatu kulia)afisa tawala mkoa wa Kilimanjaro Mashaka Juma (wa kwanza kulia) na viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Hai pamoja na madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Hai(picha na Faraja Ulomy)