Boma Hai FM

Diwani masama kusini kujenga jiko jipya shule ya Msingi Nkwamaku

22 January 2026, 5:56 pm

Pichani ni Diwani wa kata ya Masama Kusini Mhe. Cedric Benjamini Pangani (Katikati) akiwa na waalimu na wajumbe wa kamati ya shule ya msingi Nkwamakuu (Picha na Henry Keto)

Diwani wa kata ya Masama Kusini akerwa na ubovu wa jiko la kupikia chakula cha wanafunzi katika shule ya Msingi Nkwamakuu, ameahidi kuvunja na kujenga jiko jingine.

Na Henry Keto, Hai-Kilimanjaro

Wananchi wa kitongoji cha Nkwamakuu kata ya masama kusini kilichopo wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wameshukuru serikali kwa kusikiliza changamoto zilizopo kwenye kitongoji chao kwa kipindi cha muda mrefu na kuahidi kutoa ushirikiano kwa  serikali  katika kutatua changamoto zinazo wakabili, Changamoto zilizotolewa mbele ya Diwani wa kata ya Masama Kusini Mhe. Cedric Benjamini Pangani ni pamoja na uchakavu wa miundombinu katika shule ya msingi Nkwamakuu ambayo ni jiko la kupikia chakula cha wanafunzi, vyoo, stoo pamoja na uhitaji wa darasa moja

Sauti ya Mzazi na Mjumbe wa shule ya Msingi Nkwamakuu Eveta Ngowi akizungumza wakati wa ukaguzi wa jiko na vyoo katika shule ya msingi Nkwamakuu

Nae mwenyekiti wa Kitongoji cha Nkwamakuu ndugu Jorome Lema ametoa ombi kwa serikali kuitupia jicho shule ya Nkwamakuu kwa ukarabati wa majengo na huduma za msingi ili iendelee kuongeza ufaulu zaidi,pia amewataka wananchi wa kitongoji na wakazi wa maeneo ya karibu na shule kuwa walinzi wa mali za shule pamoja na kuzuia mifugo inayoingia katika eneo la shule.

Sauti ya Mwenyekiti wa kitongoji cha Nkwamakuu Jorome Lema akizungumza wakati wa ukaguzi wa jiko na vyoo katika shule ya msingi Nkwamakuu.

Pichani ni Diwani wa kata ya Masama Kusini Mhe. Cedric Benjamini Pangani akizungumza na waalimu pamoja na wajumbe wa kamati ya shule ya msingi Nkwamakuu (Picha na Henry Keto)

Kwa upande wake diwani wa kata ya masama Kusini Mhe. Cedric Pangani amepokea changamoto zilizotajwa na wajumbe wa shule na amekiri kuwepo kwa ubovu wa jiko la shule ambalo limekuwa kero kubwa katika shule hiyo, amesema jiko hilo litabomolewa na kujengwa jiko jipya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na ofisi ya mbunge wa jimbo la Hai.

Ameongeza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi hivyo wahakikishe wanatunza miti inayopandwa kwenye maeneo ya shule, ikiwa ni pamoja na kutolisha mifugo kwenye maeneo ya shule.

Sauti ya Diwani wa kata ya Masama Kusini Mhe. Cedric Pangani akizungumza wakati wa ukaguzi wa jiko na vyoo katika shule ya msingi Nkwamakuu.

Pichani ni Diwani wa Kata ya Masama Kusini (katikati) akiwa na Mtendaji wa kijiji cha Mungushi (kulia mwenye nguo nyeupe) pamoja na Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nkwamakuu (Kushoto mwenye Nguo nyekundu) (Picha na Henry keto).

Pangani amewapongeza waalimu na wafanyakazi wote wa shule kwa juhudi kubwa wanayofanya yakutoa elimu akisema ualimu ni wito kutoka kwa mungu hivyo waendelee na moyo huo huo, sambamba na hilo amezungumza na wanafunzi wa shule hiyo akiwasihi kuendelea kujisomea kwa bidii ili kukuza ufaulu zaidi kwenye shule hiyo.