Boma Hai FM
Boma Hai FM
20 January 2026, 12:13 pm

DC Bomboko ametembelea miradi mbali mbali inayoendelea kutekelezwa Wilaya ya Hai akiwa na viongozi wa dini, makundi ya kijamii ikiwemo wamachinga, Baraza la Wazee, maofisa wasafirishaji pamoja na viongozi wa Halmashauri, kwa lengo la kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Na Juma Robert
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mheshimiwa Hassan Omary Bomboko, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa soko la Mula kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa ili wananchi wa wilaya ya Hai waweze kunufaika na mradi huo.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu huyo wa wilaya wakati wa ziara iliyowahusisha viongozi wa dini, makundi ya kijamii ikiwemo wamachinga, maofisa wasafirishaji, Baraza la wazee pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai ,Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Hai ambapo jumla ya miradi mitano imetembelewa.
Mkuu wa Wilaya ya Hai amesema Serikali imejipanga kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika na kuleta tija kwa wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa mkandarasi kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa ubora unaostahili.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Mheshimiwa Edmund Rutaraka, amesema mradi wa Soko la Mula ni chachu ya maendeleo mapya na utaimarisha uchumi wa mwananchi mmoja mmoja pamoja na kuiweka wilaya ya Hai katika ramani ya masoko ya kisasa nchini.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara, katibu wa wamachinga wilaya ya Hai Joseph Venatus, ameishukuru serikali kwa kuwajengea mazingira bora ya kufanya shughuli zao za kibiashara, akisema mradi huo utasaidia kuboresha maisha ya wafanyabiashara na kuongeza fursa za kiuchumi.
