Boma Hai FM
Boma Hai FM
18 January 2026, 8:11 am

Pichani ni madarasa ya shule ya sekondari Mondo Memusi iliyopo wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.(picha na Bahati Chume)
Ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Mondo Memusi katika kijiji cha Donyomurwak wilayani Siha umeondoa changamoto ya umbali kwa wanafunzi wa jamii ya wafugaji huku Serikali ikiahidi kuharakisha usajili wake ili kuanza kutoa huduma rasmi za elimu.
Na Bahati Chume Siha-Kilimanjaro
Jamii ya wafugaji wa Kijiji cha Donyomurwak wilayani Siha mkoa wa Kilimanjaro imeiomba Serikali kuharakisha usajili wa shule mpya ya Sekondari ya Mondo Memusi ili ianze kutoa huduma kamili za elimu.
Wananchi wamesema ujenzi wa shule hiyo utapunguza changamoto kubwa ya umbali kwa wanafunzi waliokuwa wakitembea hadi kilometa 24 kila siku kwenda na kurudi katika Shule ya Sekondari Sekirari. Wamesema ndoto ya kusoma karibu sasa imetimia.

Ombi hilo limetolewa Januari 17, 2026 katika hafla fupi iliyofanyika Kijiji cha Oloiwang wakati Shirika la Mondo UK kwa kushirikiana na Mondo Tanzania likikabidhi rasmi shule hiyo kwa Serikali baada ya ujenzi kukamilika ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya ya Siha Christopher Timbuka.
Mmoja wa wananchi Paulina Israel amesema wanafunzi walikuwa wakiamka saa kumi usiku kutokana na umbali hali iliyosababisha uchovu kuchelewa masomo na changamoto nyingine ikiwemo mimba kwa watoto wa kike. Amesema wananchi walianzisha ujenzi wa shule hiyo hadi hatua ya msingi kabla ya Mondo UK na Mondo Tanzania kusaidia kwa kujenga madarasa manne ofisi mbili za walimu vyoo 12 na kutoa meza na viti 100.
Mkuu wa Wilaya Christopher Timbuka amesema Serikali itaharakisha usajili wa shule hiyo ndani ya mwezi Januari 2026 ili kuanza kuhamisha wanafunzi kutoka Sekondari ya Sekirari.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilayani humo Alfred Mosi amelipongeza Shirika la Mondo UK kwa mchango wake katika maendeleo ya elimu na kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan.
Awali mdau wa maendeleo Meijo Laizer amesema jumla ya miradi iliyotekelezwa katika vijiji vya Donyomurwak na Oloiwang imegharimu zaidi ya shilingi milioni 200 na kuishukuru Mondo UK na Mondo Tanzania kwa kuwekeza kwenye elimu.