Boma Hai FM
Boma Hai FM
29 November 2025, 10:01 am

Bodi ya Maji Uroki Bomang’ombe imehitimisha ukaguzi wa kila mwaka wa vyanzo na miundombinu ya maji katika Wilaya ya Hai, lengo ikiwa ni kuhakikisha miradi ya maji inakuwa endelevu na maji yanayotolewa kwa wananchi ni salama, na huduma ya maji inaendelea kuboreshwa.
Na Elizabeth Mafie Hai -Kilimanjaro
Kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye vyanzo vya maji pamoja na miundombinu husaidia kubaini maeneo yenye changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha huduma kwa wananchi.

Akizungumza Novemba 28 ,2025 katika kikao cha tathmini ya ukaguzi wa miundombinu kilichofanyika katika Ofisi za Bodi ya Maji Uroki Bomang’ombe kata ya Romu wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, Mhandisi Rogers Marandu amesema tathmini hiyo inalenga kuhakikisha miradi ya maji inabaki kuwa endelevu huku akisisitiza kuwa ukaguzi wa mara kwa mara unasaidia kubaini maeneo yenye changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha huduma kwa wananchi.

Ameeleza kuwa katika tathmini hiyo wamekuwa wakichunguza kwa kina ubora wa maji kwa kuhakikisha yanayotoka kwenye vyanzo na mitandao ya usambazaji ni safi na salama kwa matumizi ya binadamu. Aidha, ukaguzi huo unahusisha kufuatilia matumizi ya dawa zinazotumika kutibu maji ili kubaini iwapo zinatumika kwa usahihi na kwa kiwango kinachotakiwa.

Amesema hatua hizi ni muhimu katika kulinda afya za wananchi na kuhakikisha huduma inayotolewa inakidhi viwango vinavyotakiwa.

Mhandisi Marandu ameongeza kuwa timu hiyo imekuwa ikitembelea miundombinu ya maji ili kujiridhisha kama ipo salama na kufanya kazi ipasavyo, sambamba na kuainisha makosa na dosari zilizojitokeza katika mwaka husika na kwamba taarifa hizo hutumika kupanga marekebisho na maboresho kwa msimu ujao ili kuhakikisha mfumo wa usambazaji maji unaendelea kuwa imara, thabiti na wenye manufaa kwa jamii ya Wilaya ya Hai.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Bodi ya Maji Uroki Bomang’ombe, Batista Mngullu amesema kupitia tathmini hiyo wamejifunza kusema ukweli, kutambua makosa na kuyafanyia maboresho huku akitoa rai kwa watumishi wote wa Bodi ya Maji Uroki kuwa na ari ya utendaji ili kuendelea kuwa bodi bora na ya mfano katika utoaji wa huduma kwa jamii.
Wakizungumza katika kikao hicho baadhi ya watumia maji wa bodi hiyo wamesema ushirikishwaji wa jamii husaidia bodi kupata taarifa mapema iwapo kuna chanzo kimepata hitilafu huku wakiipongeza Bodi ya Maji Uroki Bomang’ombe kwa juhudi za kudhibiti magonjwa hatari yanayosababishwa na maji yasiyo salama kama typhoid, kipindupindu, polio na amoeba.