Boma Hai FM

Floresta Tanzania yahitimisha safari ya miaka 20 ya kuhudumia jamii wilayani Moshi

13 November 2025, 9:16 am

Pichani ni mkuu wa wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava(aliyevalia nguo ya dark blue )akiwa na viongozi mbalimbali wa shirika la Floresta Tanzania katika hotel ya African Flowers Himo mkoani Kilimanjaro(picha na Elizabeth Mafie)

Shirika lisilo la Kiserikali Floresta Tanzania limehitimisha shughuli zake rasmi katika wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na kufanya hafla ya aina yake katika hoteli ya African Flowers Himo.

Na Elizabeth Mafie Moshi -Kilimanjaro

Shirika la Floresta Tanzania  limehitimisha rasmi safari yake ya miaka 20 ya kutekeleza shughuli za kuhifadhi mazingira na kuinua maisha ya wananchi wa wilaya  ya Moshi, Novemba 12 ,2025 katika hafla iliyofanyika katika Hoteli ya African Flowers Himo mkoani Kilimanjaro.

Hafla hiyo  iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali, viongozi wa taasisi za dini, wadau wa maendeleo pamoja na wanufaika wa miradi mbalimbali ya shirika hilo na wananchi, iliyobeba kauli mbiu isemayo “Tumehitimu,jukumu la kutunza mazingira liendelee “

Akizungumza katika hafla hiyo, mkuu wa wilaya ya Moshi,  Godfrey Mnzava ambaye alikuwa  mgeni rasmi amelipongeza shirika hilo kwa kazi kubwa ya miaka 20 iliyochangia kurejesha uoto wa asili, kukuza kipato cha wananchi na kuimarisha maadili ya kiroho.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Moshi Godfrey Mzanva

“Nichukue fursa hii kuwapongeza Floresta kwa kwa kazi kubwa mliyofanya na ambayo mmeendelea kuifanya katika safari ya miaka ishirini ya ufanyaji kazi yenu katika wilaya yetu ya Moshi,hongereni sana kwa mafanikio makubwa ambayo mmeyapata”Godfrey Mzanva.

Pichani ni wanufaika wa miradi mbali mbali ya Floresta Tanzania wakiwa katika hafla hiyo iliyofanyika katika hotel ya African Flowers Himo.(picha na Elizabeth Mafie)

Nae mwenyekiti wa Bodi ya  Floresta Tanzania mchungaji  Winford Mosha amesema ujio wa shirika hilo umeleta mabadiliko makubwa na kwa haraka na kwamba wana vikundi 95  na wanashuhudia matunda ya kazi za vikundi hivyo pamoja na maelfu ya miti iliyopandwa,vyanzo vya maji vimehifadhiwa na kwamba maisha ya watu yamebadilika kupitia vikundi vya kuweka akiba na kukopa pamoja na kuwa na mahusiano mazuri na Mungu.

Pichani ni wanufaika wa miradi mbali mbali ya Floresta Tanzania wakiwa katika hafla hiyo iliyofanyika katika hotel ya African Flowers Himo.(picha na Elizabeth Mafie)

“Tulifurahia sana ujio wa shirika la Floresta Tanzania kwenye jamii yetu,ujio ambao umeleta mabadiliko makubwa ,tena kwa haraka na leo tuna vikundi 95 na tunashuhudia matunda ya kazi zao ,maelfu ya miti imepandwa na vyanzo vya maji vimehifadhiwa na maisha ya watu yamebadilika “ Mchungaji Winford Mosha

Sauti ya mwenyekiti wa shirika la Floresta Tanzania Mchungaji Winford Mosha.

Floresta Tanzania ilianza kazi mwaka 2004, ikiwa na lengo la kupunguza umaskini na kulinda mazingira kupitia programu tatu kuu,ikiwemo makuzi ya Kiuchumi,uhifadhi wa mazingira , na makuzi ya Kiroho.

Pichani ni mkuu wa wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava(aliyevalia nguo ya dark blue )akiwa na viongozi mbalimbali wa shirika la Floresta Tanzania katika hotel ya African Flowers Himo mkoani Kilimanjaro(picha na Elizabeth Mafie)

Katika kipindi hicho, shirika limefanya kazi kwenye kata 10 za wilaya ya Moshi na kuanzisha vikundi  95 vya  kuweka na kukopa  vyenye wanachama zaidi ya 2,500, kupanda zaidi ya miti 200,000 kila mwaka, na kutoa elimu ya kilimo hai kwa mamia ya wakulima.

Shughuli  hizo za kuhitimisha shughuli zake rasmi katika wilaya ya Moshi  zilipambwa na maonesho ya bidhaa, burudani za muziki kutoka kwa Zablon Singers kutoka kanda ya ziwa pamoja na ushuhuda wa mafanikio kutoka kwa wakulima, shule, na taasisi za dini zilizonufaika na kazi za shirika hilo.

Kwa miaka 20, Floresta Tanzania imekuwa nguzo muhimu katika kuibadilisha Moshi kuwa mfano wa utunzaji wa mazingira na maendeleo endelevu huku wanafuika wa miradi hiyo wakisema kuwa shirika hilo limebadilisha maisha yao kwa ujumla na kwamba wanajukumu la kuyaendeleza kwa weledi yake yote waliyoanzishiwa na Shirika la Floresta Tanzania.