Boma Hai FM
Boma Hai FM
1 August 2025, 6:25 pm

Wananchi wa Kijiji cha Kware kilichopo kata ya Masama Kusini wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wameaswa kuachana na matendo kinyume na maadili na uvunjifu wa amani unaosababisha watu kukosa usalama wao na mali zao,pamoja na kuacha matumizi ya madawa ya kulevya na pombe kali.
Na Henry Keto,Hai-Kilimanjaro
Viongozi wa serikali ya kijiji cha Kware Wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wamekemea vikali vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani katika jamii huku wakitoa tahadhari ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa wahusika watakaobainika.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa kijiji hicho, Mwenyekiti wa kijiji cha Kware Sabastian Kimaro amesema kuwa serikali haiko tayari kuona watu wachache wakishiriki katika vitendo vya uvunjifu wa amani na kutoa onyo kali kwa wanaofanya vitendo hivyo.

Kauli ya Kimaro imejiri wakati afisa mtendaji wa kijiji hicho Edwine Lamtey alipotoa taarifa ya matukio ya uhalifu katika kijiji hicho ambapo amesema kuwa kumeshamiri matukio ya wizi mdogo mdogo, uchomaji wa nyumba katika kitongoji cha Boma Kati pamoja na kujeruhiwa kwa mwenyekiti wa kitongoji cha kengele matendo ambayo sii mazuri katika jamii.
”Shida moja tunaoneana aibu, tukio anafanya mtoto wa mjomba tunamlinda! Naomba niwaambie ukweli hawa vijana wanaotusumbua ni kwamba tuliwalea sisi na tukiwaona hapo kijiweni wanakula mirungi na kucheza korokoro asubuhi mpaka jioni hatujiulizi hela wanatoa wapi; Leo nitangaze tu litapita fagio la wiki ya amani kwenye hiki kijiji kama una mtoto mdokozi au mla mirungi na mvuta bangi mkanye sasa vinginevyo utamkuta polisi. “amesema Lamtey

Kwa upande wao wananchi ambao walitoa maoni katika mkutano huo wamekemea vikali uuzaji wa pombe kali na madawa ya kulevya kama bangi na mirungi vinavyopelekea vijana hao kushindwa kutimiza majukumu Yao yakifamilia na kufanya vitendo vya kihalifu kinyume na maadili.
Hata hivyo wananchi wa kijiji hicho wameahidi kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa serikali kwa kufanya doria mara kwa mara ili kubaini wahalifu, wauzaji wa Pombe Kali na Watumiaji wa madawa ya kulevya, vilevile kuwachukulia Sheria Kali wale wote wanaobainika kuwa ndio wanaovunja Sheria na kusababisha uvunjifu wa amani na maadili wachukuliwe hatua Kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
“Tumshukuru mtendaji wetu na viongozi wa kijiji hakika vitendo hivi vipo lakini tunakiri kuwa vimepungua kwa kiasi kikubwa maana hata wahalifu wenyewe wanajua ukikamatwa utawajibishwa; na tatizo hili linaelekea kumalizika kama viongozi hawa wataendelea na msimamo huu” Alisema Mohamed