Boma Hai FM
Boma Hai FM
22 July 2025, 8:40 pm

“Mhe mkuu wa wilaya kila mwaka chama kinatekeleza msingi wa saba wa ushirika kwa kuendelea kuijali jamii,na mwaka huu Mh mkuu wa wilaya tumetembelea shule hii ya msingi Ngare Mji na tunatoa madawati ambayo thamani yake ni shilingi milioni 4 ,mwaka huu chama kinaadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa”
Na Elizabeth Noel Siha –Kilimanjaro
Chama cha Akiba na Mikopo Hai Rural Teachers Saccos (HRT)kimekabidhi madawati 40 yenye thamani ya kiasi cha shilingi milioni nne katika shule ya Ngare Mji iliyopo wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro.
HRT Saccos imekabidhi madawati hayo Julai 22,2025 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa msingi wa saba wa vyama vya ushirika unaohimiza kurudisha kwa jamii faida inayopatikana ndani ya chama.

Akizungumza wakati wa kupokea madawati hayo mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Siha Shedrack Moshi ameishukuru HRT SACCOS kwa jitihada walizofanya na kuona umuhimu wa kurudisha kwa jamii na kwamba madawati hayo yanakwenda kuondoa msongamano wa wanafunzi darasani na kufanya ufaulu kuongezeka

“Ndugu zangu nipende kusema kwa niaba ya serikali kwamba tumefarijika sana na jitihada hizi ambazo zimefanywa na chama hiki ambacho kimeona umuhimu wa kurudisha kwa jamii,na leo hii wamekabidhi madawati 40 kwa ajili ya watoto wetu katika shule hii,badala ya watoto kukaa kwa kusongamana sasa hivi wataweza kukaa vizuri na hivyo ule usikivu na kama alivyohaidi mwalimu mkuu ufaulu unaenda kuongezeka”Amesema Moshi
Awali akisoma taarifa ya HRT SACCOS Mwalimu Alex Warioba ambae ni mwenyekiti wa chama hicho amesema kila mwaka chama kinatekeleza msingi wa saba wa vyama vya ushirika kwa kuendelea kuijali jamii na kwa mwaka 2025 wameona ni vyema kutoa madawati hayo ili kupunguza upungufu wa madawati uliopo katika shule hiyo.
“Mh mkuu wa wilaya kila mwaka chama kinatekeleza msingi wa saba wa ushirika kwa kuendelea kuijali jamii,na mwaka huu Mh mkuu wa wilaya tumetembelea shule hii ya msingi Ngare Mji na tunatoa ambayo thamani yake ni shilingi milioni 4 ,mwaka huu chama kinaadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa”Amesema Mwalimu Warioba.
Nae afisa elimu msingi wilaya ya Siha Fatu Msangi amesema kupitia msaada huo wa madawati yaliyotolewa na HRT SACCOS yatafanya utekeleza wa mtaala kufanyika kwa ufanisi zaidi.

“Thamani hizi mlizotupatia zitatufanya utekelezaji wa mtaala kufanyika kwa ufanisi zaidi kuliko ambavyo watoto wangekuwa wamesongamana hivyo tunawashukuru sana HRT SACCOS”Amesema Msangi
Kwa upande wao wanafunzi wa shule ya msingi Ngare Mji Sofia Yusuph na Asia Hussen wameishukuru HRT SACCOS na kuhaidi kutunza madawati hayo pamoja na kusoma kwa bidii.
Katika wiki ya maadhimisho ya miaka 25 ya HRT SACCOS imeendesha shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo michezo ya bonanza, kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari, na sasa kukabidhi madawati hayo kama sehemu ya mchango wake kwa maendeleo ya elimu nchini.