Boma Hai FM
Boma Hai FM
20 June 2025, 10:42 pm

Pichani ni mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Elinikyo Mafuwe akizindua shule ya msingi Muungano(picha na Salma Sefu)
Mbunge wa jimbo la Hai, Saashisha Mafuwe, ameweka jiwe la msingi katika shule mbili mpya ,Shule ya Msingi Muungano na Shule ya Sekondari Mbatakero zitakazosaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuondoa changamoto ya kutembea umbali mrefu,Katika hotuba yake amesisitiza nidhamu, bidii katika masomo, na kuheshimu jitihada za wazazi.,Pia amehimiza utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti katika shule hizo.
Na Elizabeth Mafie . Hai-Kilimanjaro
Wanafunzi wa Kata ya Muungano na Kata ya Weruweru, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, wameondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu na msongamano wa wanafunzi darasani, kufuatia ujenzi wa shule mpya katika maeneo hayo,kata ya Muungano imepata shule mpya ya msingi, huku Kata ya Weruweru ikipata shule mpya ya sekondari.
Akizindua shule hizo Juni 20 , 2025 mbunge Saashisha amewataka wanafunzi wa wilaya ya Hai kuwekeza katika elimu kwa bidii na nidhamu, ili kutimiza ndoto zao na kusema kuwa tayari serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu kwa ajili ya maendeleo ya watoto wa Kitanzania.
“Wanafunzi mnapaswa kusoma kwa bidii. Siri ya mafanikio katika elimu ni nidhamu Ukiona umevaa sare za shule na una vifaa vyote vya kujifunzia, tambua kuna mzazi anayejitahidi sana ,anaweza kuwa anafanya vibarua sokoni au hata kuuza mifugo ili kuhakikisha unatimiza ndoto zako,” amesema Saashisha.
Aidha, amebainisha kuwa maendeleo makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni deni ambalo wananchi wanapaswa kulilipa kwa kufanya kazi kwa bidii na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Katika hotuba yake, Mhe. Saashisha amehimiza utamaduni wa upandaji miti katika maeneo ya shule hizo, akisema kuwa mazingira mazuri ni kichocheo cha kujifunza kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Muungano, Mhe. Edmundi Rutaraka, amesema kuwa licha ya wananchi wa kata hiyo kumiliki mifugo, wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa na inalindwa dhidi ya mifugo.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa shule ya msingi ya Muungano, Mwalimu Martha Zablon amesema kuwa lengo kuu la mradi huo ni kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Msingi Kambi ya Raha, na pia kuwasaidia wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kutoka maeneo ya Mlima Shabaha na Jiweni, waliokuwa wanasoma katika shule za Kambi ya Raha, Sanya Station na Kingereka.