Boma Hai FM
Boma Hai FM
10 June 2025, 9:48 pm

Mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe ameuliza swali bungeni kuhusu lini serikali itachukua hatua ya ukarabati wa barabara ya Rundugai-Simanjiro inayounganisha wilaya ya Hai na Simanjiro
Na Henry Keto.Hai-Kilimanjaro
Mbunge wa Jimbo la Hai, Mheshimiwa Saashisha Mafue, ameonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu hali mbaya ya barabara inayounganisha maeneo ya Rundugai, Kambi ya Chokaa mpaka Simanjiro, ambayo kwa sasa haipitiki kutokana na uharibifu mkubwa unaosababishwa na mvua na sababu nyingine.
Mbunge Mafue amesisitiza kuwa hali hii imevuruga mawasiliano kati ya Wilaya za Hai na Simanjiro na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi pamoja na shughuli za kiuchumi katika maeneo haya muhimu.

Akijibu kuhusu changamoto hii, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mheshimiwa Zainab Katimba, amesema Serikali inatambua mazingira hayo na inajitahidi kushughulikia matatizo yanayojitokeza kutokana na mvua na uharibifu wa barabara.
Aidha, Naibu Waziri Katimba ameitaka TARURA mkoa wa Kilimanjaro kwa ushirikiano na mameneja wa Manyara na wilaya husika kuhakikisha tathmini ya kina ya uharibifu wa barabara hiyo inafanyika haraka ili kuandaa maombi ya fedha kwa ajili ya hatua za dharura za kurejesha mawasiliano ya barabara hiyo muhimu.
Serikali inasisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya barabara kuhakikisha mawasiliano na shughuli za maendeleo hayakatiki katika wilaya mbalimbali.