Boma Hai FM
Boma Hai FM
28 May 2025, 9:21 pm

Wahenga walisema hasira hasara,na ndivyo ilivyotokea kwa Edwin Kileo baada ya kushindwa kuzizuia hasira zake na kuchoma nyumba aliyojenga huko ukweni.
Na Elizabeth Mafie.Siha-Kilimanjaro
Mahakama Wilayani Siha mkoani Kilimanjaro,imemuhukumu Edwin Kileo mkazi wa Kijijii cha Naibili (32)ambaye ni mwinjilisti wa Kanisa moja la KKKT wilayani Siha,kwenda kutumikia miaka 15 jela kwa kosa la kuchoma moto nyumba aliyojenga kwa wakwe zake kwa sababu ya ugomvi wa kifamilia .
Mwedesha mashitaka wa serikali Kulwa Mungo mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo Jasmin Abdul,amesema tukio hilo limetokea April 19 ,2025, katika Kijijii cha Naibili wilaya ya Siha.
Mwedesha mashitaka huyo ,amesema siku ya tukio mshitakiwa huyo alifika nyumba walipokuwa wanaishi na kuingia ndani kisha kukusanya vitu mbalimbali zikiwamo nguo na kuzichoma moto ndani ya nyumba kisha kutokomea.
Kulwa amesema mwinjilisti huyo alikuwa amejenga nyumbani Kwa baba mkwe eneo la Naibili Wilaya ya Siha na kwamba ,baada ya kuhitilafiana na mkewe ,mkewe alirudi kwa wazazi wake na yeye kuondoka hivyo nyumba ikabaki bila mtu.
Baada ya jitihada za usuluhishi kushindikana ndipo Kileo alimua kujichukulia sheria mkononi kwa kuchoma moto nyumba hiyo yenye vyumba viwili kisha kutokomea kusikojulikana lakini baadae kukamatwa akiwa Bomang’ombe Wilaya Hai.
Mwendesha mashitaka ,amesema tukio hilo ni kinyume na kifungu 319(a)sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya 2022
“Ni kweli tukio hilo ni kinyume na Sheria ya kanuni ya adhabu sura 16 iliyafanyiwa marejeo 2022 na kesi namba 12572 /2025″amesema Kulwa
Kabla ya hukumu kutolewa Mwinjilisti huyo alitakiwa kijitetea baada ya kukiri tukio hilo, na kusema kwamba alifanya hivyo kutokana na kutoelewana na mke wake.
Amesema mara kadhaa amekuwa akimuomba mkewe huyo kurudi na kuendelea kulea familia yao lakini mkewe alikataa hivyo kwa hasira akaamua kufanya tukio hilo huku akiiomba mahakama kumuonea huruma kwani ana watoto wanao mtegemea.
Pamoja na maombi hayo hakimu huyo alimtaka kwenda kutumikia jela miaka 15 badala ya kifungo cha maisha baada ya kutoa utetezi wake.