Boma Hai FM
Boma Hai FM
12 May 2025, 11:55 am

Halmashauri ya wilaya ya Hai imetoa madawati mia moja kwa ajili ya shule ya msingi Kware yenye thamani ya shilingi milioni kumi.
Na Henry Keto. Hai -Kilimanjaro
Afisa mtendaji wa Kijiji cha Kware Edwin Lamtey ametoa wito kwa jamii, waalimu, wazazi, wanafunzi na wote wanaozunguka maeneo ya shule na miradi mingine kulinda rasilimali zote zinazotolewa na serikali katika kuleta maendeleo kwa jamii.
Lamtey ametoa wito huo wakati akipokea Madawati 100 kwenye shule ya Msingi kware iliyopo kata ya Masama kusini Kijiji cha Kware Yenye thamani ya Shilingi Million 10 zilizotokana na Mapato ya ndani ya halmashauri, vilevile amesema amepokea shilingi milioni 3.5 kwaajili ya ujenzi wa jiko la shule na tayari limejengwa na Milioni 6 kwaajili ya matundu ya vyoo.
Aidha ameishukuru serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa juhudi kubwa zinazofanyika kuleta maendeleo katika jamii ya watanzania kwa maslahi ya wote.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Jamaida Marcus ameishukuru serikali kwa kutoa Madawati hayo ambayo yataongeza ufanisi kwa waalimu na wanafunzi katika kutoa na kupata elimu Bora, amesema Madawati hayo yameongeza idadi ya Madawati yaliyokuwepo ambayo pia wanafunzi watakaa wawili wawili na Madawati yatabaki.
Nae mwenyekiti wa shule hiyo ameishukuru serikali kwa kutoa Madawati hayo na kuiomba pia kuangalia kwa upande wa miundombinu ya shule hiyo ambayo ni chakavu kutokana na umri mkubwa wa shule hiyo.
Wanafunzi wa shule hiyo wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa madawati ambayo yatawapa fursa ya kusoma vizuri na kuahidi kufaulu katika mitihani yao.