Boma Hai FM
Boma Hai FM
27 April 2025, 8:51 pm

Katika kuendelea kuchochea maendeleo hapa nchini Bodi ya maji Uroki Bomang’ombe yajenga matundu nane ya choo katika shule ya msingi Kiselu.
Na Gasper Mushi. Hai-Kilimajaro
Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe ameipongeza bodi ya maji Uroki Bomang’ombe kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni ishirini na tano zilizotumika kujenga matundu nane ya choo cha shule ya msingi Kiselu iliyopo kata ya Machame Uroki wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Saashisha ametoa pongezi hizo leo aprli 27 2025 wakati alipozindua matundu hayo ya choo ambayo yanakwenda kuwaondelea adha waliyokuwa wakipitia wanafunzi wa shule hiyo kutokana na choo walichokuwa wakitumia hapo awali kuwa chakavu na hata kutishia usalama wa wanafunzi hao.

“Kitendo hiki walichokifanya bodi ya maji Uroki Bomang’ombe ndio yalikuwa maono yangu, ndio yalikuwa matarajio yangu, mnaona sasa bodi hii imekuwa ikifanya ukarabati, inajenga vyanzo vipya, inatanua wigo na leo wanarudisha sehemu ya kile ambacho wamekipata na kuja kututengenezea mradi wa choo, niwapongeze sana mwenyekiti wa bodi na watendaji wote” Amesema Saashisha.
Nae mwenyekiti wa bodi hiyo Batista Mngulu amesema wamekuwa na utaratibu wakurudisha kwa jamii na lengo kubwa ni utunzaji wa mazingira kwani shule hiyo ipo karibu na chanzo cha maji saaki na kwamba wao kama wadau wa maji wanatakiwa kutoa huduma ya maji safi na salama na waliona ni jambo jema kurudisha katika eneo hilo ili kuendelea kutunza mazingira.
Mngulu amewashauri waalimu wa shule hiyo pamoja na wanafunzi kutunza matundu hayo ya choo kwa kuyafanyia usafi ili yaweze kutumika muda mrefu .

Kwa upande wake meneja wa bodi Uroki Bomang’ombe Mhandisi Anold Mbaruku amesema wamechagua kuweka mradi huo katika shule ya msingi Kiselu ili kulinda chanzo cha maji Saaki na kwamba jukumu la bodi hiyo ni kuhakikisha wananchi wanapata maji safi ,na kuwepo kwa matundu ya choo ambayo ni chakavu kunaweza kupelekea chanzo cha maji kuathirika.
Hata hivyo afisa uhusiano wa bodi hiyo ndugu Hardson Kimaro amesema shule hiyo ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa matundu ya choo hivyo wao kama bodi waliona ni vyema kupeleka mradi huo katika shule ya msingi Kiselu kwani itarejesha moyo kwa wananchi wanaozunguka katika chanzo cha maji Saaki pamoja na kuwaondoa katika hatari wanafunzi wa shule hiyo.