Boma Hai FM

DC Bomboko aungana na wadau wa maji Hai kumpongeza Rais Samia

14 April 2025, 12:25 pm

Mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko akizungumza na wadau wa maji (hawapo pichani) picha na James Gasindi.

Kutokana na mafanikio ya sekta ya maji kwa wilaya ya Hai, Mkuu wa wilaya hiyo pamoja na wadau wampongeza Rais Samia.

Na James Gasindi Hai-Kilimanjaro.

Wadau wa maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, kwa kauli moja, wamepitisha azimio la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kuimarisha huduma ya maji wilayani Hai.

Katika kikao kilichowakutanisha wataalamu, viongozi wa serikali, na wawakilishi wa wananchi, wadau hao walisema kuwa juhudi za Rais Samia zimeleta mageuzi makubwa katika sekta ya maji na kuondoa adha ya ukosefu wa huduma hiyo muhimu kwa wananchi wa Hai.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mhe. Hassan Bomboko, aliungana na wadau hao na kueleza kuwa Wilaya ya Hai imenufaika na miradi ya maji yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 9 katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia. Mafanikio hayo yamewezesha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 90 ya maeneo ya wilaya hiyo.

“Kwa sasa, suala la maji siyo changamoto kwetu tena hapa Hai. Tumeimarisha vyanzo vilivyokuwepo, tumeanzisha vyanzo vipya, na tuna uwezo wa kuzalisha, kuhifadhi na kusambaza maji kwa wananchi kulingana na mahitaji yao,” alisema.

Mhe. Bomboko alibainisha kuwa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatamka kuwa huduma ya maji vijijini itafikia asilimia 75 ndani ya miaka mitano, lakini Wilaya ya Hai tayari imepiga hatua kubwa kwa kufikia asilimia 90.

“Rais wetu ana dhamira ya kweli ya kumtua mama ndoo kichwani. Amefanya kazi kubwa inayostahili pongezi,” aliongeza.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko.

Wadau hao walisisitiza kuwa kuna umuhimu wa kutoa pongezi kwa Rais akiwa bado madarakani kama njia ya kuthamini juhudi zake.

“Waswahili wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Hapa Hai tunasema mnyonge hanyongwi na haki yake anapewa. Rais Samia anastahili pongezi,” alisema Mhe. Bomboko.

Wakati wa kufunga kikao hicho, wadau waliweka msisitizo wa kuendeleza ushirikiano baina ya wananchi na serikali katika kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inakuwa endelevu.