

9 April 2025, 9:55 am
Ikiwa ni wiki ya upandaji miti iliyoanza rasmi Aprili mosi mwaka huu,halmashauri ya wilaya ya Hai imeendelea kupanda miti sehemu mbali mbali kwa ajili ya kuendelea kutunza mazingira.
Na oliver Joel
Diwani wa kata ya Masama Kusini Cedrick Pangani amewataka wakazi wa vijiji vya Kware na Mkombozi kutunza miundombinu ya shule ya sekondari Mkombozi iliyopo katika kijiji cha Mkombozi ikiwa ni pamoja na kutunza miti elfu moja iliyopandwa jana shuleni hapo.
Akizungumza na wananchi wa vijiji hivyo waliojitokeza kwa wingi kwa ajili ya zoezi la kupanda miti shuleni hapo ,diwani Pangani amesema kuwa shule hiyo ni manufaa kwa wananchi wa masama kusini kwa ujumla na si kijiji cha Mkombozi pekee,hivyo kila mwananchi anapaswa kutunza miundombinu ya shule hiyo ikiwa ni pamoja na kutunza miti hiyo kwa kuepuka kupeleka mifugo katika eneo hilo la shule lililopandwa miti.
Naye afisa maliasili wa wilaya ya Hai John Katikiro amesema kuwa lengo la kupanda miti elfu moja shuleni hapo ni utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi kupanda miti katika taasisi za uma pamoja na utunzaji wa mazingira,ambapo pia amewataka wakazi wa Hai kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kwa kupanda miti katika maeneo yao.
Naye katibu wa umoja wa wazazi Ccm Benard Gisunte amesema kuwa wananchi wanapaswa kutunza vyema miundombinu ya shule hiyo ikiwa ni pamoja na kutunza miti hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Naye mwenyekiti wa kijiji cha Kware Sebastian Kimaro amesema kuwa atashirikiana vyema na wananchi wake kuhakikisha kuwa wanatunza vyema shule hiyo kwani shule hiyo ni inayoitwa Mkombozi imekuwa mkombozi kwa wanafunzi waliokuwa wanatembea umbali mrefu kwenda katika shule ya sekondari ya mukwasa.