Boma Hai FM

Pad. Dkt. Aidan aadhimisha siku ya kuzaliwa kwa kugawa miche ya miti

30 March 2025, 8:40 am

Padre Dkt Aidan aliyevaa kofia akiwa na wadau mbali mbali wa mazingira katika shule ya sekondari Mawenzi katika siku yake ya Kuzaliwa(picha na Elizabeth Mafie)

Wakati baadhi ya watu duniani wakisheherekea siku zao za kuzaliwa kwa kukata keki,imekuwa tofauti kwa Padre Dkt Aidan kwa kugawa miche ya miti zaidi ya elfu moja kwa taasisi mbali mbali kwa lengo la kuboresha mazingira.

Na Elizabeth Mafie

Mkurugenzi na mwanzilishi wa Taasisi ya mazingira na Maendeleo Kilimanjaro KCDE padre Dkt Aidan Msafiri ameadhimisha kutimiza miaka 62 kwa kugawa miche zaidi ya elfu moja   ya  miti ya matunda kwa taasisi mbali mbali za serikali na binafsi ikiwemo shule ya sekondari Mawenzi.

Zoezi hilo la upandaji wa miti limefanyika wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro chini ya usimamizi wa Dkt Aidan Msafiri ambapo ametoa wito kwa jamii licha ya kuadhimisha siku zao za kuzaliwa kwa kukata keki watumie siku hizo katika kuifanya dunia iwe ya kijani.

Sauti ya Padre Dkt Aidan mkurugenzi na mwanzilishi wa taasisi ya mazingira na maendeleo Kilimanjaro(KCDE)

Frank Ngowi ambae ni makamu mkuu wa shule ya sekondari Mawenzi amesema ni adhma ya Mh.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuona watanzania wanatumia nishati safi na nishati bora na kwamba ndio  wadau wanasisitiza kuacha matumizi ya kuni na mkaa ili kuyatunza mazingira.

Sauti ya makamu mkuu wa shule ya sekondari Mawenzi Mwalimu Frank Ngowi.
Makamu mkuu wa shule ya sekondari Mawenzi akipanda mti(picha na (Elizabeth Mafie)

Ameongeza kuwa kwa kupanda miti mingi na utunzaji wa mazingira ni kumuunga mkono  Mh.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan  katika jitihada zake za kuboresha Mazingira.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Muungano Athman Msuya amemshukuru Padre Aidan kwa kuwapatia Miche 200 ya miti  na kusema wanafunzi wanahitaji kivuli,matunda,hewa safi,mvua ili kuweza kuboresha mazingira ya shule.

Sauti ya mwalimu mkuu shule ya msingi Muungano Athman Msuya.

Amesema kuwa wanaahidi kuitunza miti hiyo vizuri na kuhakikisha inakuwa yote kwa manufaa ya shule na jamii inayo wazunguka .