

27 March 2025, 8:36 pm
Kutokana na kuwepo kwa ajali nyingi zinazotokana na waendesha bodaboda, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Jimbo la Hai wamekutana na kuzungumza na waendesha bodaboda hao kwa lengo la kuhakikisha wanabaki salama.
Na Elizabeth Mafie
Maafisa wasafirishaji wametakiwa kuwa waaminifu pamoja na kuepuka mambo maovu,na kuheshimu alama na sheria za usalama barabarani ili kupunguza ongezeko la ajali za mara kwa mara zinazo hatarisha maisha yao.
Hayo yameelezwa na Mchungaji Mathayo Stanley Mtui ambaye ni Katibu wa idara ya vijana na wanafunzi Dayosisi ya Kaskazini wakati alipo muwakilisha msaidizi wa askofu katika mkutano uliowakutanisha madereva boda boda ama maofisa wasafirishaji wilayani Hai mkoani Kilimanjaro uliofanyika katika usharika wa Hai mjini ( KKKT )Dayosisi ya Kaskazini Jimbo la Hai.
Mchungaji Mathayo amewashauri maofisa wasafirishaji kufanya mambo ya maana ikiwa ni pamoja na Kuwa waaminifu , kuepuka uhalifu jambo ambalo litasababisha kuingia katika mkono wa sheria pamoja na kuhatarisha Usalama wao na hata wakati mwingine kutumikia kifungo gerezani.
Aidha ameongeza kuwa wanapaswa kuzingatia alama za barabarani kwa lengo la kuepukana na ajali zitakazo sababisha kupata ulemavu wa kudumu.
Sambamba na hayo amewataka maofisa usafirishaji waliopata fursa ya kuhudhuria mkutano huo kuwa mawakala kwa kutoa Elimu kwa wenzao ili kuwa na madereva boda boda wenye uelewa wa namna ya kujikinga na ajali,kudumisha uaminifu baina yao na wateja.
Kwa upande wake mkuu wa jimbo la Hai mchungaji Binieli Malyo amewataka maofisa Wasafirishaji kujali afya zao lakini pia kujali afya za wateja wao.
Akizungumza katika mkutano huo amesema Ili wateja waendelee kutumia huduma zao yawapasa Kuwa waaminifu kwa kujali Afya zao na za Wateja wao kwa kuepuka Vitu vyote ambavyo ni hatarishi.
Meneja wa Benki Of Afrika Tawi la Moshi (BOA)Mpoki Mwanjara amesema kulingana na kuwa Boda Boda wanatafuta kipato cha kila siku wameona unafuu wao upo katika kuweka malengo ya fedha,kuiheshimu pamoja na kutunza kwenye akaunti ambazo hazina gharama na zitakazo wapa faida.
Aidha amesema lengo kuu ni kuhakikisha kuwa Boda Boda anafikia Malengo yake kwa kupitia kipato anachokipata Kila siku Lakini anajua namna sahihi ya kuhifadhi Fedha, kupitia uhamasishaji wa akaunti mbali mbali mfano BOA ambazo hazina gharama za uendeshaji lakini pia zinawapa faida.
Maofisa wasafirishaji nao wakapata fursa ya kueleza namna walivyo nufaika na mkutano huo huku waki shukuru kanisa la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Jimbo la Hai kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kwa kuwathamini na kuona umuhimu wa wao kupata elimu ya usalama Barabarani.