Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
13 March 2026, 7:47 pm

Polisi wanawake mkoa wa Morogoro wamefanya harambee ya kupata kiasi cha fedha Tsh.630,000 kusaidia matibabu baada ya kuona uhitaji kwa mtoto Zuhaira mara baada ya kumtembelea March 6,2026 wakiadhimisha siku ya wanawake Duniani
Na Katalina Liombechi
Mtandao wa Polisi Wanawake mkoa wa Morogoro umetoa msaada wa shilingi 630,000 kwa ajili ya matibabu ya mtoto mwenye ulemavu, Zuhaira Libenanga, mwanafunzi wa shule ya sekondari Katindiuka katika Halmashauri ya mji wa Ifakara.
Akizungumza hii leo March 13,2026 akiwa katika shule ya Sekondari Katindiuka wakati wa kukabidhi fedha hizo Mkuu wa Sayansi Jinai Wilaya ya Kilombero kwa niaba ya Polisi hao wanawake amesema Msaada huo umetolewa baada ya mtandao huo kuambiwa uhitaji wa kiasi cha Tsh 300,000 na mama mzazi wa mtoto huyo mwenye umri wa miaka 13 walipomtembelea tarehe 6 Machi 2026, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo Katika ziara hiyo pia walimkabidhi mahitaji mbalimbali pamoja na kiti mwendo.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Zaituni Omary, amesema Zuhaira alizaliwa bila ulemavu wowote, lakini alianza kupata tatizo hilo akiwa darasa la tano bila sababu inayofahamika na alipatiwa matibabu, lakini hakurejea katika hali yake ya kawaida.
Ameeleza kuwa kama familia ilishindwa kuendelea na matibabu kutokana na changamoto za kifedha, hivyo msaada huo wa fedha utasaidia kufanikisha matibabu ya mtoto wake.

Kwa upande wake, Zuhaira ametoa shukrani kwa msaada alioupata na kusema utampa matumaini zaidi katika safari yake ya matibabu na masomo.
Nao Yasinta Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Katindiuka pamoja na Mratibu elimu wa Kata hiyo Rehema Mahecha wamesema msaada huo ni faraja kubwa kwa mwanafunzi huyo na utamsaidia kuendelea na masomo yake kwa urahisi zaidi.
