Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
7 March 2026, 11:09 am

Mto Ikwambi ulikuwa hatarini kutoweka kutokana na uharibifu wa mazingira uliosababishwa na shughuli za kibinadamu
Na Katalina Liombechi
Shirika la Kilombero Organization for Community Development (KOCD) limefanikiwa kurejesha uhai wa Mto Ikwambi uliopo katika Kijiji cha Sululu, Kata ya Signali, baada ya kutoweka kwa takribani miaka nane kutokana na shughuli za kibinadamu.
Mafanikio hayo yamepatikana kupitia mradi wa SUSTAIN-ECO unaofadhiliwa na Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori Afrika (AWF) kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) chini ya ufadhili wa Serikali ya Sweden, ukiwa na lengo la kurejesha mifumo ikolojia katika Bonde la Kilombero.
Akizungumza baada ya kikao kazi cha siku mbili cha wanamtandao wa vinara wa uhifadhi wa Bonde la Kilombero kilichofanyika Machi 5–6, 2026 katika Ukumbi wa Ecological Monitoring Centre Mang’ula, Afisa kutoka KOCD Abdalah Kisung’a amesema juhudi za urejeshaji wa mto huo zimefanikiwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Awali Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ikwambi ameeleza kuwa baada ya mto huo kuharibiwa ilikuwa ikiwaathili katika shughuli za kilimo kwani mapato yalikuwa kidogo ukilinganisha na siku za nyuma na kwamba kwa sasa wamekuwa na matumaini makubwa ya kuongeza kipato kupitia kilimo kutokana na uwepo wa maji ya kutosha.
Katika ziara ya mafunzo iliyofanywa na wana mtandao wa Kilombero network of conservation champions (KNCC) katika eneo la mto huo, Mwenyekiti wa mtandao huo Ibrahim Ndembo amesema mafanikio ya KOCD ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya jamii na wadau mbalimbali katika kulinda na kurejesha rasilimali za asili.

Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Salome Mayenga amesema juhudi za uhifadhi wa vyanzo vya maji ni muhimu kwa maendeleo ya miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, ambalo zaidi ya asilimia 65 ya maji yake yanategemea Mto Kilombero.

Katika hatua nyingine, wanamtandao hao walitembelea na kushiriki zoezi la upandaji miti katika ushoroba wa Nyerere–Udzungwa, eneo muhimu la mapito ya wanyamapori mradi ambao umetekelezwa na shirika la Southern Tanzania Elephant Program (STEP) kwa kushirikiana na serikali ambapo KNCC wamepanda miti zaidi ya 1,000 katika ushoroba huo.

Picha ya eneo ya vinara wa KNCC wakipanda miti eneo la Ushoroba wa Nyerere-Udzungwa(Picha na Katalina Liombechi)
Kupitia mafunzo hayo ya vitendo, wanamtandao wa uhifadhi wamepanga kuendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za uhifadhi ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kuhusu upandaji miti, kuhamasisha kilimo endelevu, kuanzisha njia mbadala za kipato na kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Kikao kazi hicho kilichofadhiliwa na AWF kililenga kuimarisha ushirikiano na kupanga mikakati ya kuendeleza juhudi za uhifadhi wa mazingira katika Bonde la Kilombero.