Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
3 March 2026, 7:15 pm

Miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za serikali katika kuboresha sekta ya elimu, miundombinu jumuishi na rafiki kwa makundi yote.
Na Katalina Liombechi
Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Mheshimiwa Abubakar Asenga, leo ametembelea Kata ya Lumemo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara ambapo amepokelewa kwa shangwe na wananchi waliojitokeza kwa wingi kumsikiliza na kuwasilisha kero zao.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Asenga ameeleza mafanikio ya miradi iliyotekelezwa ndani ya siku 100 chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa Serikali imeendelea kuwaletea wananchi maendeleo yenye tija na yanayogusa maisha yao ya kila siku.
Miongoni mwa miradi iliyotekelezwa ni ujenzi wa madarasa mawili pamoja na matundu sita ya vyoo maalum kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Lumemo Wenye thamani ya zaidi ya Tsh. Mil 55.
Awali akisoma taarifa ya Mradi huo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lumemo Nelson Ngewe amesema Mradi huo umefanikiwa chini ya Fedha za BOOST ukilenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuhakikisha watoto wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum, wanapata haki yao ya elimu katika mazingira salama na rafiki.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo, Mheshimiwa Asenga alieleza dhamira ya serikali kuwa imekusudia kuleta ujumuishi katika sekta zote kwa kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo bila ubaguzi akisisitiza kuwa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za serikali katika kuboresha sekta ya elimu, miundombinu na huduma za kijamii.

Pamoja na mambo mengine Mh. Asenga ameahidi kukabidhi tenki la maji lenye ujazo wa lita elfu tano la kuhifadhia maji kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum ikiwa ni miongoni mwa changamoto zilizoelezwa.